Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limesema linashirikiana na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar kuandaa mafunzo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kabla ya kuanza rasmi kwa vikao vya Bunge hilo Jumanne ya wiki
ijayo. Pia,
limesema linashirikiana na baraza hilo kuandaa stahiki, ambazo wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba watapasa kuzipata kutokana na nafasi zao za
ujumbe wa Bunge hilo.
Katibu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashililah
(pichani), alisema hayo jana alipotakiwa na NIPASHE kueleza kama kuna
mambo yaliyoandaliwa, kama vile mafunzo kwa wajumbe wa Bunge hilo baada
ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Jambo lingine, ambalo Dk. Kashililah alitakiwa na NIPASHE kueleza ni
stahiki zipi, ambazo wajumbe wa Bunge hilo, ambazo watapasa kupata.
Dk. Kashililah alisema: “Tunashirikiana na Katibu wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kufanya maandalizi. Tutatoa taarifa.” Rais Kikwete
alisema Bunge hilo litachukua siku 70, lakini lisipomaliza kazi yake kwa
muda uliopangwa, litaongezewa siku nyingine 20.
Tayari Rais Jakaya Kikwete amekwishateua watu 201 kutoka makundi
mbalimbali ya kijamii, yakiwamo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali,
vyama vya siasa na taasisi za kidini kuwa wajumbe wa Bunge hilo.
Wajumbe hao wataungana na wabunge 358 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na wajumbe 76 wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuunda
Bunge Maalumu la Katiba.
CHANZO: NIPASHE