Shirika
la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), jana lilizindua mabasi mapya 175
na kufanya mabasi yaliyopo kufikia 288 yatakayokuwa yanatoa huduma ya
usafiri katika jiji la Dar es Salaam huku Wizara ya Uchukuzi ikiliagiza
kuwa la kwanza kuingia katika mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Darts) kwa
kuwa ina vigezo. Mabasi
hayo ni kati ya 1,000 yaliyonunuliwa na kampuni ya Simon Group ambayo
inamiliki UDA ambayo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu yatakuwa
yamewasili nchini.
Mwenyekiti
Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group ambayo inamiliki shirika hilo,Robert
Kisena, alimweleza Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba,
kuwa shirika hilo limepanga kununua mabasi mengine 2,000 na kufikisha
idadi ya mabasi 3,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kisena
alisema ujio wa mabasi hayo utaleta changamoto kubwa katika jiji la Dar
es Salaam na kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao wamekuwa wakigombania
kupanda katika daladala kutokana na uchache wa mabasi.
“Vijana
wengi wakimaliza masomo na kupata kazi wanakimbilia kuwaza kununua
magari japo ajira hakuna, kwa hiyo tunataka kujenga utamaduni watu
wayatumie mabasi yetu kwa shughuli mbalimbali ili wasiwe na haja ya
kununua magari,” alisema.
Kisena alisema mpango wa muda mrefu ni kwamba ifikapo Juni mwaka huu UDA
itaanza kutoa huduma ya usafiri katika mikoa ya Mwanza na Mbeya na pia
yatanunuliwa mabasi yatakayotoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam
kwenda mikoa mingine.
Dk. Tizeba, alisema UDA iwe ya kwanza kuingia katika mradi wa mabasi
yaendayo kasi ambao ujenzi wa barabara zake unaendelea vizuri katika
jiji la Dar es Salaam kwa kununua mabasi makubwa yatakayokuwa na uwezo
wa kuchukua abiria wengi.
Alisema kumekuwa na tatizo mashirika na makampuni yanapobinafsishwa kwa
watu binafsi wanayaendesha kwa muda mfupi na baada ya kubadili malengo
ya awali na kwamba serikali itakuwa inawachukulia hatua wanaofanya
hivyo.
Dk. Tizeba alisema serikali inapata hasara kubwa kwa siku kutokana na
tatizo la foleni linalojitokeza katika jiji la Dar es Salaam na ndiyo
maana inafanya kila inavyowezekana jiji hili linakuwa na huduma za
usafiri za kila aina.
CHANZO: NIPASHE