Mbunge mmoja
wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati, ambaye alikuwa katika mstari wa mbele
kupinga mauaji ya Waislamu nchini humo, ameuawa kwa kupigwa risasi
katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui. Jean-Emmanuel
Ndjaroua aliuawa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliokuwa
wakitumia pikipiki, siku moja tu baada ya kutoa hotuba kulaani mauaji
yanayoendelea nchini humo.
Msemaji
wa shirika la kutetea haki za kibinadam la Human Rights Watch, Peter
Bouckaert ameonya kuwa hali nchini humo inaendelea kuwa mbaya kila uchao
na raia wote wa nchi hiyo ambao ni Waislamu huenda wakalazimika
kutoroka katika kipindi cha wiki chache zijazo.
Maafisa wa
kutoa misaada ya kibinadam wamesema kuwa watu tisa wamefariki dunia
kufuatia mapigano makali na uporaji uliotokea katika mji mkuu jamuhuri
ya afrika ya kati wikendi iliyopita.
Ripoti zinasema kuwa watu wawili wanaoaminika kuwa waislamu waliuawa kinyama wakati wa machafuko hayo.
Vita vikali
vilitokea siku ya Jumamosi kati ya wanamgambo wa Kikristo na Waislamu
Magharibi mwa mji mkuu wa Bangui ambapo majengo kadhaa yaliharibiwa kwa
kuteketezwa.
Mapigano yaendelea katika sehemu kadhaa
Mkaazi mmoja
wa Bangui alisema kuwa mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kumuua mama mmoja
Mkristu aliuawa na mwili wake kuchomwa na umati nje ya ukumbu wa baraza
la mji huo.
Wanamgambo
wengine wa Kikristu walimuua mtu Muumini mwengine wa Kiislamu na wakati
umati ulipokuwa ukijiandaa kuuteketeza mwili wake, wanajeshi wa Rwanda,
ambao ni sehemu ya kikosi cha jeshi la kutunza ambani ya Muungano wa
Afrika, MISA walifika mahala hapo na kumpiga risasi.
Watu wengine watano waliuawawa kati hali isiyojulikana.
Peter
Bouckaert wa shirika la kutetea haki za kibinaadamu alithibitisha mauaji
hayo na kuongeza kuwa mtu mwingine aliuawa kinyama siku ya Jumapili
karibu na soko kuu mjini Bangui.
Bwana
Bouckaert alisema kuwa majeshi ya Rwanda wamemueleza kuwa hali katika
CAR inawakumbusha mauaji ya halaiki iliyotokea nchini mwao miongo miwili
iliyopita.
Jamuhuri ya
Afrika ya Kati imekumbwa na mapigano kwa karibu mwaka moja sasa tangu
kundi la waasi la Seleka lilipomteua Michel Djotodia kuwa rais wa kwanza
Muislamu kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo machi mwaka wa elfu mbili
kumi na tatu.
Mapigano
hayo yameendelea hata baada ya Djotodia kujiondoa na bunge kumuidhinisha
Catherine Samba Panza kuwa kaimu rais wa nchi hiyo mwezi uliopita na
waislamu wamekuwa wakitoroka mapigano hayo kwa maelfu.
Afisa huyo
mwandamizi wa shirika la kutetea haki za kibinaadamu ameiambia BBC
kwamba baada ya siku au majuma machache Waislamu wote wataihama Jamhuri
ya Afrika ya Kati.
Chanzo - BBC Swahili