Wakati Rais Jakaya Kikwete akijiandaa kwenda London Uingereza
kuhudhuria mkutano wa kuokoa viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani
ukianza wiki hii, tatizo la ujangili limeweka wingu zito kwa Tanzania. Rais Kikwete ni kati ya viongozi wa nchi 50 watakaohudhuria mkutano huo, utakaokuwa chini ya wenyeji wa mwana wa Wales na Waziri wa Mkuu wa Uinegerza, David Cameron,
Taarifa ya gazeti la The Mail on Sunday la
Uingereza la Februari 8, limeitaja Tanzania kama kinara wa ujangili kwa
kuua zaidi ya tembo 11,000 kwa mwaka, huku Rais wake (Jakaya Kikwete)
akielezwa kufumbia macho.
Pia, gazeti
hilo limemhusisha Rais Kikwete kuwa na urafiki na wafanyabiashara ya
meno ya tembo, huku likiwahusisha wafadhili wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
katika biashara hiyo.
“Utawala wa
Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo yaliyovunja rekodi katika
historia ya nchi yake. Kibaya zaidi, wahifadhi wanasisitiza kuwa, ndani
ya Serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo,” imesema sehemu ya
taarifa hiyo.
Katika
mkutano huo, viongozi wa nchi 50 na mawaziri wataweka mikakati dhidi ya
biashara haramu ya wanyamapori, yenye thamani ya pauni 6 bilioni za
Uingereza kwa mwaka zinazotumika kufadhili magaidi.
Taarifa hiyo inasema kuna wafanyabiashara wakubwa wa Dar es Salaam wanaohusika na ujangili.
“Miongoni
mwao ni matajiri wakubwa nchini, wafadhili na wanachama wa CCM na ndugu
wa karibu wa Rais Kikwete. Lakini wanao marafiki wakubwa, huku majaji,
waendesha mashtaka na polisi hurubuniwa kwa urahisi,” inasema sehemu ya
taarifa hiyo.
Pia, taarifa
hiyo inadai kuwapo kwa idadi kubwa ya Wachina wanaofanya biashara ya
mafuta nchini, huku baadhi yao wakihusika na ujangili.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu alikiri kuona taarifa hiyo na
kwamba, Rais Kikwete atahudhuria lakini aliipuuza taarifa hiyo.
“Ni kweli Rais Kikwete atahudhuria huo mkutano, lakini taarifa ni ya None sense, crap and malicious (ya kishenzi, kipuuzi na ovu),” alisema Rweyemamu.
Juhudi za
kumpata Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu hazikufanikiwa
baada ya simu yake kuita muda mrefu bila kupokelewa.
Hata Naibu wake, Mahmoud Mgimwa naye hakupokea simu alipopigiwa.
Kuhusu CCM
taarifa hiyo imeitaja idara ya wanyapori kunuka rushwa huku ikisingizia
kuuzwa kwa meno ya tembo yaliyoko ghalani kwenye soko la kimataifa
wakati lengo lao ni kupata fedha kuisaidia chama hicho uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015.
“ Wabunge,
maofisa wa juu na wafanyabiashara, wametajwa bungeni na kwenye vyombo
vya habari, lakini uchunguzi unapotezwa,” inaongeza. Jitihada za kupata viongozi wa CCM hazikuzaa matunda.
Chanzo - Mwananchi