
Licha ya
ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama kutarajiwa kufikia katika
hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo atakapowasili nchini Julai
Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa tahadhari ya vyakula ambavyo
hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni pamoja na kutumia maji ya
bomba.
Mbali
na tahadhari hiyo, ziara hiyo ya Obama itakuwa na ulinzi mkubwa ambao
pengine haujawahi kutokea katika historia ya viongozi wa nje
wanaotembelea Tanzania kwani utahusisha idadi kubwa ya magari, ndege za
kijeshi na meli kubwa ya kivita ambazo zitakuwa zikifanya doria karibu
na pwani ya Tanzania.
Tahadhari za
matumizi ya chakula, maji na nyinginezo zimetolewa katika nchi zote
tatu za Afrika ambazo Obama atatembelea, kila moja kwa jinsi Wamarekani
hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi - Vyombo
vya usalama vya Marekani vimejipanga kuhakikisha ziara ya kiongozi huyo
haivurugwi kwa namna yoyote ile. Tayari ndege za jeshi zilizobeba
magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’ maalumu kwa ajili
ya kiongozi huyo, yamewasili katika nchi hizo tatu za Afrika
atakazotembelea.
Kwa mujibu
wa gazeti la Washington Post la Marekani, ndege hizo pia zimebeba malori
matatu ambayo yamesheheni karatasi maalumu za kuzuia risasi kupenya
kwenye vioo, zitakazobandikwa kwenye madirisha ya hoteli ambazo Rais
Obama na ujumbe wake watafikia.
Kwa mujibu
wa gazeti hilo, mamia ya mashushushu wa Marekani tayari wako katika nchi
hizo. Meli maalumu za kubeba ndege za kivita, maarufu kwa jina la
‘amphibious ship,’ ikiwa na hospitali maalumu na yenye vifaa vyote
itaweka nanga baharini, jirani na nchi atakayokuwa Rais Obama, tayari
kukabiliana na dharura yoyote itakayotokea. Gazeti hilo liliandika kuwa
ndege za kivita za Marekani zitakuwa zikipeana zamu kufanya doria kwa
saa 24, katika anga la nchi ambayo Rais Obama atakuwepo, iwapo ndege za
‘adui’ zitakaribia eneo linaloitwa ‘anga ya rais.’ Kwa mujibu wa gazeti
hilo, ziara ya Rais Obama aliyoifanya hivi karibuni katika nchi za
Ujerumani na Ireland Kaskazini, japo kulikuwa na gharama kwa walinzi,
lakini safari za nchi za Afrika zimeelezwa kuwa na gharama kubwa zaidi.
Tahadhari- Kwa
mujibu wa taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya Marekani, ambayo Mwananchi
imepata nakala yake, watu watakaokuwa kwenye msafara wa Obama wametakiwa
kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia maji ya chupa zaidi.
“Kutokana na
mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu wetu kutumia maji ya chupa zaidi
kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa kuelewa
fika tatizo la ugonjwa wa malaria nchini, ujumbe wa Obama umeshauriwa
kutumia dawa ya mbu ya kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.
Deet ni dawa
maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na
kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye vita
mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka
1957.
ATM nazo noma - Pia
watu watakaokuwa kwenye msafara wa Rais Obama wametakiwa kuhakikisha
wanatumia mashine za kutolea fedha (ATM) zilizoko karibu na hoteli
watakazofikia.
“Kuna tatizo
la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri kutumia ATM ambazo ziko katika sehemu
zisizo salama. Pia katika kipindi watakachokuwa Tanzania watu wanapaswa
kutumia teksi ambazo zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia siyo
vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye vyumba mtakavyolala. Pia kina
mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa wanapita
mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.
Chanzo - Mwananchi



