Mwenyekiti wa
Tume ya Katiba, Ali Saleh Ali, amewataka wajumbe wa mabaraza ya katiba
ngazi za wilaya, wasiogozwe na ‘mawazo fungwa’ wakati wa kutoa maoni yao
kuhusu uboreshaji wa rasimu ya katiba.Ali ametoa tahadhari hiyo juzi
baada ya kutokea mvutano mkali kati yake na baadhi ya wajumbe wa baraza
la katiba wilaya ya Singida, wanaohudhiria kikao cha baraza la katiba
kinachoendelea kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Wananchi mjini
hapa.Mvutano huo ulisababishwa na baadhi ya wajumbe kudai kuwa
mwenyekiti huyo, alikuwa akifanya utetezi mkubwa ulioonyesha kila dalili
kwamba una ushawishi wa moja kwa moja wa kutaka wajumbe hao wapitishe
kila kitu kilichomo kwenye rasimu ya katiba.Baada ya kubanwa, mwenyekiti
Ali alisema “Wajumbe naona mmekuja hapa tayari mkiwa na ‘mawazo fungwa’
kitu ambacho kinasababisha tushindwe kuelewana”.
Bila
kufafanua zaidi juu ya mawazo hayo fungwa, mwenyekiti huyo alisema kuwa
kwa utaratibu, ni lazima mjumbe anayeuliza swali ni lazima ajibiwe papo
hapo.Lakini kwa upande wa maoni,maoni yanachukuliwa kama yalivyo na
kupelekwa mbele.Ali alisema kwa sababu kuna wajumbe waliokuja na mawazo
fungwa,wanapata tabu ya kuafikiana wanapojadiliana.“Kwa kifupi ni kwamba
hakuna maoni ya mjumbe yeyote yatakayoachwa au kukataliwa, mnayo fursa
kubwa kila mjumbe kueleza maoni yake anayoona yatasaidia kupata katiba
ya ustawi wa kizazi cha sasa na kile kijacho,”alisema.Mmoja wa wajumbe
wa kikao hicho, Elia Digha, alitoa duku duku lake kuwa tume ya katiba
imekuja Singida kukusanya maoni na si kutetea rasimu kama alivyoonyesha
mwenyekiti.Katika hatua nyingine, asilimia kubwa ya wajumbe wa kikao
waliungana na Watanzania wengine wanaopinga kuundwa Serikali tatu.
Wamedai
Serikali tatu italeta madhara mengi ikiwemo gharama kubwa ya uendeshaji
na pia itachangia kuzorota kwa undugu uliojengeka kwa miaka mingi.
Aidha,wamepiga kipengere cha kuruhusu wagombea binafsi kwa madai utachangia mafisadi kutumia mwanya huo kupata uongozi.



