
Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida) itaanza kutoa vitambulisho kwa wananchi wa
kawaida wa Mkoa wa Dar es Salaam, kutokana na zoezi la uandaaji wa
vitambulisho hivyo kuwa katika hatua za mwisho. Hayo
yalisemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati cha Nida,
Thomas William, alipokuwa akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es
Salaam.
William
alisema wananchi watatakiwa kwenda kuweka picha na alama ya dole gumba
katika Serikali za Mitaa yao kwani taarifa zao kamili zipo katika
uongozi wa mitaa yao.
Pia alisema kuwa vitambulisho hivyo vitatumika katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka ni na baadaye Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Zoezi la ugawaji vitambulisho limeanzia kanda ya Mashariki na watumishi
wa umma 220,000 wamekwishapatiwa vitambulisho hivyo na jumla ya wakazi
wapatao milioni tatu wa Mkoa wa Dar es Salaam watapatiwa vitambulisho
hivyo.
Zoezi la usajili wa wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya
taifa ulikamilika katika Mkoa wa Dar es Salaam Julai mwaka jana. Lengo
la Nida ni kutaka kila Mtanzania anapatiwa kitambilicho cha taifa na
kukitumia katika uchaguzi wa 2015.
SOURCE: NIPASHE



