Siku
zote tunaamini kuwa mtu anapofariki hupumzika kwa amani, lakini siku
hizi wafu hao hawapumziki tena kwa amani, bali huamshwa, kisha, wafu
wengine kushika nafasi zao.
Ni
kama vile muda wa marehemu hao kukaa kaburini umekwisha hivyo, nafasi
zao zinatakiwa kutumiwa na wengine kutokana na uhaba wa maeneo ya
kuzikia.
Maeneo
mengi ya kuzikia katika Jiji la Dar es Salaam, hasa yale maarufu kama
Kinondoni, Sinza, Temeke na Kisutu yanapendwa zaidi na watu na sasa
yamefurika.
Kujaa kwa maeneo haya ya kuzikia kumesababisha makaburi ya watu wengine, kufukuliwa kisha kutumika kuzikia miili mingine.
Hata hivyo, makaburi ambayo
hufukuliwa ni yale ambayo hayajajengewa, yametelekezwa, hayana kitu
chochote cha kuonyesha kuwa kuna kaburi pale au mengine hayana alama
kama misalaba au imeondolewa.
Msemaji
wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Kaiohela anasema kuwa anafahamu
kwamba makaburi hayo yamejaa, lakini hakutaka kuzungumza zaidi akitoa
ahadi kuwa siku ya Jumatatu atalifikisha suala hilo kwa wahusika wakuu.
Katika
makaburi ya Temeke Chang’ombe, Mwananchi Jumapili lilishuhudia makaburi
yakiwa yamesongamana kiasi ambacho ni vigumu mtu kupata nafasi ya
kuweka mguu.
Mlinzi
wa makaburi hayo, Athuman Mtembwe anasema kutokana na ufinyu wa nafasi
katika makaburi hayo, makaburi ambayo hayana alama yoyote ni rahisi
kufukuliwa na kuzikiwa kwa mara nyingine.
“Mimi
kama mlinzi wa eneo hili ninaweza kukutafutia sehemu ambayo unaweza
kuchimba kaburi, lakini kama hufahamu utafukua tu maiti nyingine,”
anasema
Anasema
kuwa mara kwa mara watu wanaokuja kuchimba makaburi ili kuzika ndugu
zao, wamekuwa wakifukua miili ya watu wengine ambayo makaburi yao
hayakuwa na alama yoyote.