
MJANE
wa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten, marehemu
Daudi Mwangosi, Itika Mwangosi anatarajia kukabidhiwa Sh milioni 10 kama
kifuta machozi. Itika, atakabidhiwa fedha hizo katika maadhimisho ya
siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yatakayofanyika jijini
Arusha kuanzia Mei 3 hadi 5, mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi, Tumaini Mwailenge alisema fedha hizo, zitamsaidia mjane huyo
kuanzisha miradi atakayoona inamfaa katika maisha yake.
Alisema mbali ya fedha
hizo, utazinduliwa mfuko maalum utakaojulikana kwa jina la Daudi
Mwangosi Fund, ambao utakuwa unasaidia kila mwandishi pale anapopata
matatizo.
“Mtakumbuka Septemba 2,
2012 mwandishi wa kituo cha Chanel Ten, marehemu Daudi Mwangosi aliuawa
katika Kijiji cha Nyololo, wakati polisi wakipambana na wafuasi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Sasa tumeona ni vema
tukatoa kifuta machozi kwa mjane wa marehemu Mwangosi, ili aweze
kuanzisha miradi yoyote ya biashara na katika maadhimisho ya mwaka huu
tutazindua mfuko maalum wa kusaidia waandishi,” alisema.
Alisema maadhimisho hayo, yataadhimishwa ngazi ya Afrika Mashariki, ambapo nchi zote tano zitajumuika pamoja jijini Arusha.
Alisema mada
zitakazojadiliwa katika maadhimisho hayo, ni usalama na mazingira bora
ya waandishi wa habari Afrika Mashariki, maboresho na mabadiliko ya
vyombo vya habari juu ya utendaji kazi.
Nyingine ni haki za binadamu kwa waandishi wa habari nchini Tanzania na hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Alisema baada ya
majadiliano hayo, litapitishwa azimio la pamoja la waandishi wa habari
Afrika Mashariki na kuongeza kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni usalama
wa mwandishi wa habari sehemu ya kazi.
Alisema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera.
Katika mkutano wa jana,
wawakilishi kutoka vyama vya waandishi wa habari na taasisi walihudhuria
na kuzungumzia hali ya usalama wa mwandishi na mazingira yake ya kazi.
Baadhi ya vyama hivyo ni
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri (TEF), Umoja wa wanahabari wa
kimataifa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).
Nyingine ni Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN) na Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA).
habari NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM
Picha - chingaone library
chanzo - mtanzania



