Ndege aina ya Cessna 5H-QTT ikiwa imeanguka eneo la Kisongo, karibu
na Uwanja wa Ndege Arusha juzi jioni, baada ya kugonga mti wakati
ikijiandaa kutua na kusababisha kifo cha mmiliki wake na aliyekuwa
rubani, Bob Sambeke(katika picha ndogo juu). Picha na Filbert Rweyemamu.
KWA UFUPI Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha,
Ester Dede alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea kufanywa na
wataalamu wawili wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga kutoka Dar es Salaam.
Arusha.
Wakati mazishi ya mfanyabiashara bilionea wa Moshi, Ernest Babu
‘Sambeke’ yakiwa yamepangwa kufanyika keshokutwa, msiba wake umekuwa wa
kitajiri kutokana vyakula na vinywaji kumwagwa kwa wingi nyumbani kwa
marehemu.
Msiba wa mfanyabiashara huyo uko nyumbani kwake, Njiro – Themi nje
kidogo wa Mji wa Arusha ambako habari zinasema mamia ya watu wamekuwa
wakifurika kuhani.
Matajiri wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wakiwa na magari ya kifahari
wamefurika katika msiba huo na habari zaidi zinasema mamilioni ya
shilingi yamechangwa kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya bilionea huyo
aliyefariki dunia, Jumamosi iliyopita kwenye ajali ya ndege.
Ajali hiyo ilitokana na ndege aina ya MT 7- yenye namba 5H-QTT ambayo
alikuwa akiiendesha mwenyewe kuanguka kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha,
baada ya bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na
uwanja huo.
Alifariki dunia wakati askari magereza waliompa msaada walipokuwa
wakimkimbiza hosipitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na
majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.
Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede alisema uchunguzi wa ajali
hiyo unaendelea kufanywa na wataalamu wawili wa Mamlaka ya Usafiri wa
Anga kutoka Dar es Salaam.
Magari makubwa yaliyosheheni vyakula na vinywaji yamekuwa yakiingia na
kutoka katika makazi ya Sambeke ambako waombelezaji wote wameandaliwa
maeneo maalumu ya kuketi yaliyofunikwa na mahema ambako vinywaji na
vyakula vinatolewa.
Msemaji wa familia, Dk Richard Masika alisema marehemu atazikwa katika
eneo la Karanga mjini Moshi ilipo nyumba yake na kwamba misa itaanza saa
7.00 mchana katika Kanisa Katoliki mjini Moshi na mazishi kufanyika saa
10.00 jioni.
Habari zaidi zilizopatikana zinaeleza kuwa marehemu atazikwa akiwa
amevalia sare za marubani kutokana na kupenda kwake kurusha ndege.
Habari zaidi zinasema familia ya marehemu imekuwa ikifuatilia mali
alizokuwa nazo marehemu zikiwemo fedha wakati akipatwa na mauti.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema, Babu Sambeke
alikuwa ni rafiki wa watu wengi, wakiwapo wanasiasa wa vyama vyote.
“Binafsi baada ya kupata taarifa za kufariki kwa Babu Sambeke,
niliwapigia baadhi ya wabunge na mawaziri, wote walishtushwa sana na
msiba huu,” alisema Nassari.
Babu Sambeke ni mmoja wa wafanyabiashara wa kwanza katika kanda ya
Kaskazini kumiliki ndege, na hadi anafariki alikuwa akitumia ndege
mbili.Jina lake lilianza kuwa maarufu 1985 akionekana kama mtoto wa
mjini `mission town’ na baadaye alijiimarisha kibiashara na kuwa na
utajiri mkubwa.