Baada
ya kuonya wananchi wanaotumia dawa za tiba mbadala ambazo
hazijathibitishwa, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania(TFDA), sasa
inawataka wananchi kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa kunywa kama dawa.
Akizungumza
juzi katika Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam,
msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema Mamlaka hiyo ilipima na
kubaini mafuta hayo yana tindikali ya mafuta.
Alifafanua
katika maonesho hayo maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja
vya Mwalimu J.K. Nyerere, kwamba mafuta hayo hayafai kuliwa na binadamu
na anayekunywa kwa wingi, yuko hatarini kupata saratani za aina tofauti
tofauti.
"Hivi
karibuni kumekuwa na wimbi la wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu
kama dawa, kwa kuwaelekeza wananchi kunywa. Napenda kuwataarifu kuwa
mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta," alisema.
Mwandishi
alipata sampuli ya vielelezo vya matumizi yake na manufaa yake mwilini,
kama inayotangazwa na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali na hata
katika mitandao.
"Ni
mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu {au kokwa}. Hukamuliwa kiini chake
na kutoa mafuta. Yana ubora kuliko mafuta mengine ya kupikia, yana
Vitamin A, B, C, D na F. Pia yanatibu magonjwa mbalimbali," kielelezo
kimoja kilinadi ubora wake katika mitandao ya jamii.
Mafuta
hayo yamedaiwa kutengeneza seli zote ndani ya mwili, kuzuia ngozi
isiharibike wala kupata makunyanzi, kuondoa mafuta ndani ya mishipa ya
damu na yanapunguza uzito uliozidi.
Pia
inadaiwa yanarutubisha ini na figo, yanaleta hamu ya kula, yanaimarisha
mifupa, kucha na nywele, yanaongeza kinga ya mwili (CD4), yanaondoa
sumu na yanatengeneza sukari iwe katika kiwango kinachotakiwa.
Maelezo
hayo yameendelea kusifu kwamba yanasaidia kuona vizuri na kujenga
kumbukumbu, yanapunguza vitambi na matumbo makubwa, yana virutubisho
vyote vinavyohitajika mwilini.
Katika
ngozi yametajwa kuondoa madoa, chunusi, fangasi, upele, mba na muwasho,
yanafaa kwa walemavu wa ngozi (albino). Pia huondoa hamu ya kutumia
dawa za kulevya na kuponyesha vidonda vya tumbo.
"Endelea
kutumia mafuta bora ya ubuyu, ni bidhaa asilia ya kitanzania. Ni mafuta
yasiyochanganywa na kitu chochote, ni mafuta asilia," yamesifiwa
katika maelezo hayo.
Mtumiaji
ameelezwa kama ana ugonjwa wa kisukari, atumie kijiko cha chakula
kimoja tu. Anatakiwa kutumia dozi hiyo ya kwanza nusu saa kabla ya kula
chochote kwa muda wa siku 15.
Dozi
ya pili na ya tatu kwa wagonjwa hao, inatakiwa kufuata baada ya siku 15
kisha mgonjwa apumzike wiki moja, huku akiendelea kupima kila wiki.
Kipimo hapo ni cha hospitali.
Kwa
wagonjwa wa vidonda vya tumbo, figo na ini, wameelekezwa na
wajasiriamali hao kunywa kijiko cha chakula kimoja asubuhi kabla ya kula
chochote, na usiku kijiko cha chakula kimoja kabla hajala chochote kwa
muda wa siku 15 kwa dozi ya kwanza.
Baada
ya hapo, mgonjwa anapumzika wiki moja kisha siku 15 zinazofuata dozi ya
pili, mapumziko wiki moja halafu siku 15 nyingine dozi ya tatu.
Maelezo
ya dozi hiyo ya kutibu ugonjwa wa vidonda vya tumbo, yanaendelea
kumtaka mgonjwa baada ya dozi ya tatu, aanze kunywa kila wiki mara moja
kijiko cha chakula kimoja asubuhi, tena nusu saa kabla hajala chochote
kwa muda wa wiki nne.
Dozi
inaendelea ambapo mgonjwa atatakiwa kunywa kijiko kimoja cha chakula
kila mwezi mara moja asubuhi, kabla hajala chochote kwa muda wa wiki
nne, kisha kunywa kila mwezi mara moja, asubihi kabla hajala chochote
kwa muda wa miezi sita mfululizo.
Kwa
utoaji wa sumu, mgonjwa ametakiwa kunywa kijiko cha chakula kimoja
asubuhi kila siku kwa muda wa siku 14, kisha kunywa kila mwezi mara moja
kwa muda wa miezi sita mfululizo.
Kwa
kuongeza CD4 mwilini, ametakiwa kupata kijiko cha chakula kimoja
asubuhi nusu saa kabla ya kula chochote, na usiku kijiko cha chakula
kimoja nusu saa kabla ya kula chakula cha usiku kwa muda wa miezi
mitatu.
"Mgonjwa
aanze kunywa baada ya kipimo cha mwisho (cha CD4) alichopima. Mafuta
yanapatikana kuanzia ujazo wa lita moja na zaidi," imesifiwa dawa hiyo.
TFDA
imeonya kuibuka kwa tabia ya wananchi kutaka matibabu ya haraka, kama
ilivyo kwa baadhi ya watu kutaka utajiri wa haraka, na imehadharisha ni
vema kabla ya kutumia dawa zinazoibuka kila siku, waulize kama zina
ubora kwa afya zao.
"Nawasihi
wananchi kuacha kukimbilia dawa ngeni mara tu baada ya kutangazwa kama
haya Mafuta ya Ubuyu, yamekuwa yakielezwa ni dawa na wajasiriamali tu,
na wengi wamekuwa wakitumia bila kusikiliza mamlaka husika zinasemaje,"
alisisitiza.
Semwanza
alisema Mamlaka hiyo iko katika mkakati wa kuanza kuelimisha jamii
kuhusu matumizi ya mafuta hayo, ambayo wengi wanayaamini na kuyanywa
kama dawa.
Kwa
mujibu wa Semwanza, baada ya kupima mafuta hayo na kubaini hatari hiyo,
waligundua pia inawezekana tindikali hiyo kutenganishwa na mafuta hayo,
lakini imebainika utaalamu na teknolojia hiyo haipo nchini.
Hata hivyo, alisema Mamlaka hiyo haijabaini madhara ya matumizi mengine ya mafuta hayo kama kipodozi.
Kutokana
na mvuto huo wa kibiashara, na shauku ya kupona haraka ya wananchi,
Semwanza alisema TFDA imekuwa ikifanya msako wa dawa mbalimbali
zinaouzwa na wajasiriamali katika maonesho hayo.
Alisema
kuwa kuna baadhi ya waandaaji wanaowaalika wajasiriamali bila kufuata
kanuni na sheria za kuingiza dawa hizo katika maonesho.
Kwa
mujibu wa Semwanza, wanakagua dawa na kama wakikuta hazijathibitishwa
na TFDA na mamlaka nyingine, wanamuamuru mjasiriamali kuacha kuzitangaza
mpaka apate kibali na kuwaasa wanaowaleta wajasiriamali katika maonesho
hayo ya kimataifa kuhakikisha wanafuata vigezo.
Wiki
iliyopita TFDA, ilionya wananchi dhidi ya matumizi ya dawa za tiba
mbadala, zikiwamo zinazokuza maumbile, ambazo bado hazijasajiliwa na
Mamlaka hiyo baada ya kuchunguza usalama, ubora na ufanisi wa dawa hizo.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa, ilitoa nafasi ya watoa tiba mbadala kwenda kusajili dawa zao, lakini mwitiko umekuwa hafifu.
TDFA
yenye dhamana ya kusimamia ubora na usalama wa bidhaa za vyakula na
dawa, ikiwa ni pamoja na dawa za mitishamba, vipodozi na vifaa tiba
vinavyouzwa katika soko la Tanzania, imeeleza kuwa watoa huduma wa tiba
mbadala, wengi hawako tayari kubainisha aina ya mchanganyiko wa dawa
hizo jambo ambalo ni hatari kwa walaji.