Mchumi
wa CCM, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Shadrack Mwanjuguja akidhibitiwa na
vijana baada ya kutokea vurugu jana asubuhi katika Kijiji cha Ruanda2
wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Santilya, Mbeya Vijijini.
Picha ndogo ni Mkuu wa Polisi Kituo cha Kati, Mbeya, Richard Mchomvu
akimsindikiza hospitali Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji
Lackson Mwanjale baada ya kujeruhiwa katika kata hiyo. Picha na Godfrey Kahango
Wabunge
wawili, mmoja wa CCM na mwingine wa Chadema, jana walikula vichapo
walipokuwa katika harakati za uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika
katika kata 27 nchini. Wabunge
hao, Godbless Lema (Chadema) wa Arusha na Mchungaji Jackson Mwanjele wa
Mbeya Vijijini walipata vipigo katika matukio tofauti yanayohusiana na
uchaguzi huo.
Lema
alidai kuwa alinusurika kifo kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa
polisi na ilibidi aanguke chini na kujifanya amezirai ili kujiokoa,
katika tukio lililotokea jana jioni, eneo la Shule ya Sombetini
alipokuwa akielekea katika kituo cha kupigia kura.Mara
baada ya kufika jirani na kituo cha Sombetini, inadaiwa kuwa polisi
walisimamisha gari ya Lema na kuanza kumuhoji lakini ghafla ilitokea
kutoelewana kipigo kuanza. Katika tukio hilo, Lema alipata kipigo hadi
kuangukia katika mfereji na akiwa chini, alionekana kama amezimia hivyo
polisi walimuachia na kuokolewa na wafuasi wa Chadema.
Akizungumza
baada ya tukio hilo, Lema alisema bila kujifanya amezirai angeweza
kuuawa... “Wamenipiga sijui kosa langu, mimi kama mbunge niliitwa na
mawakala wakiomba gari kubeba masanduku na ni kweli nilikuwa nimewasha
taa za gari nikishangilia. Kesho naenda kupimwa hospitali kwani nina
maumivu kwenye mbavu. Baada ya hapo nitajua cha kufanya kwani
walionipiga nawajua.”
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea tukio
hilo lakini mmoja wa polisi waliokuwa eneo la vurugu hizo, alisema
walilazimika kimdhibiti Lema, kwani alikuwa anafanya fujo jirani na
kituo cha kura.
“Hakuna aliyempiga, alianguka mwenyewe kwenye mfereji, tulimtaka aondoke kwa amani akagoma,” alisema askari huyo.
Mbeya Vijijini - Mchungaji
Mwanjale kwa upande wake, aliumizwa baada ya kupigwa na kundi
linalodaiwa kuwa la wafuasi wa Chadema, katika Kitongoji cha Shipongo,
Kijiji cha Ruanda, Mbeya wakati yeye na makada wengine wa CCM walipofika
hapo wakiwa kwenye gari la chama hicho.
Mbunge huyo
alivuja damu nyingi kichwani na mashuhuda wa tukio hilo walisema kabla
ya kupigwa, kulikuwa patashika baina ya walinzi wa CCM na wale wa
Chadema waliokuwa wakilinda kura katika uchaguzi huo.
Mchungaji
Mwanjale inaelezwa kuwa alijiokoa baada ya vijana hao walipomwacha na
kuanza kumshambulia Mchumi wa CCM, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Shadrack
Mwanjuguja ambaye alikuwa amefuatana naye.
Baada ya
kuponyoka, Mwanjale alikimbilia kwenye nyumba moja iliyopo karibu na
vijana hao walimfuata na kugonga kwa nguvu ili waingie ndani, lakini
alitoroka kupitia mlango wa nyuma kisha kuruka uzio wa nyumba hiyo huku
Mwanjuguja akiwekwa chini ya ulinzi.
Mbunge huyo
na mwenzake waliokolewa na polisi wa doria waliokuwa wakiongozwa na Mkuu
wa Polisi wa Wilaya (OCD) Mbeya, Richard Mchomvu ambaye aliwachukua na
kuwapeleka Kituo cha Afya Kilembo kwa ajili ya matibabu.
Daktari wa
kituo hicho, Franco Anthony alisema Mchungaji Mwanjale alipigwa na kitu
kizito kichwani na kushonwa nyuzi tatu huku mwenzake Mwanjuguja
akishonwa nyuzi mbili kichwani.
Baada ya
kupata matibabu walikwenda Kituo cha Polisi Mbalizi kufungua jalada la
mashtaka. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema watu
saba walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Vurugu Bagamoyo - Vurugu
ziliibuka katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Magomeni, Bagamoyo
na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi baada ya watu
wanaodhaniwa ni wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema kuwashambulia wa
CCM.
Katika
vurugu hizo zilizotokea saa mbili asubuhi, inadaiwa zaidi ya wafuasi 15
wa CCM walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Mkuu wa
Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kwamba kuwa watu kadhaa walikamatwa huku polisi wakiendelea na
uchunguzi.
Lindi - Msimamizi
wa Uchaguzi Kata ya Namikago, Wilaya ya Nachingwea, Valery Kwembe
alimtangaza Alferd Mhagama wa CCM kuwa mshindi kwa kura 511 dhidi ya
Hamisi Chingole wa Chadema (188), Hamis Malipiche wa CUF (110) na
Belisimas Mbinga wa ADC (1).
Katika Kata
ya Kiwalala CCM imeibuka mshindi baada ya Sheneni Zahoro kupata kura
1,158 akifuatiwa na wa CUF, Shazil Mosha 803 na Mboga Hassan wa Chadema
90.
Moshi - Katika
Kata ya Kiborloni, Moshi, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Erasmo Silayo
alimtangaza Frank Kagoma wa Chadema kuwa mshindi kwa kupata kura 1,019
dhidi ya 255 za Willy Tulli wa CCM. Mgombea wa UDP, Aidan Mzava
aliambulia kura mbili.
Iringa - Kata ya Ibumu,
(Iringa), Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Justine Mgina alimtangaza
Hemed Mbena wa CCM kuwa mshindi kwa kura 891 dhidi ya kura 338 za July
Petro wa Chadema.
Tanga - Msimamizi
wa Uchaguzi, Juliana Malange alimtangaza mgombea wa CCM, Kauli Makame
kuwa ameshinda Kata ya Kiomoni kwa kura 857 dhidi ya mgombea CUF Mwaruko
Omary aliyepata kura 451 wakati mgombea wa Chadema Mwanaisha Omary
alipata kura 132.
Katika Kata ya Mtae Lushoto, mgombea wa CCM Hamza Mohamed amepita bila kupingwa baada ya wagombea wa vyama vingine kujitoa.
Njombe Mjini - Mgombea
wa Chadema katika Kata ya Njombe Mjini hiyo, Agrey Mtambo aliibuka
kidedea kwa kupata kura 2,202 dhidi ya mpinzani wake wa CCM Menard Mlyuka aliyepata kura 1,094.
Kiteto - Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Partimbo, Kiteto- Arusha, Nevil Kimolo alimtangaza mgombea wa CCM, RaphaelNangole kuwa mshindi wa kura 837 dhidi ya mpinzani wake wa karibu kutoka Chadema Saning’o Kornei aliyepata kura 587.
Mbeya - Msimamizi
Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Malindo, Stephen Mwakingwe alimtangaza
mgombea wa CCM, Nelson Mwaikambo kuwa mshindi kwa kura 747 dhidi ya
Nicodemus Mwakalile wa Chadema aliyepata kura 408 wakati mgombea wa TLP,
Raphael Mwakabanga alipata kura 51.
Mbeya Vijijini - Katika Kata ya Santilya, Msimamizi wa Uchaguzi, Raphael Mwangunga
alimtangaza mgombea wa CCM, Anthony Mboma kuwa mshindi kwa kura 1,650
na kumshinda Elisha Mwandele wa Chadema aliyepata kura 1,154.
Shinyanga - Katika
matokeo ya udiwani Kata ya Ubwage, Hamisi Majogoro wa CCM ameibuka
kidedea baada ya kupata kura 323 akifuatiwa na Adam Ngoma wa Chadema
aliyepata kura 219 na Majika Lubinza wa Tadea aliyepata kura 95.
Morogoro - Mgombea
wa CCM, Mzelu Paul aliibuka mshindi kwenye Kata ya Tungi baada ya
kuwashinda wagombea watano. Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi huo, Jelvis
Simbeye alisema Mzelu alipata kura 715 akifuatiwa na Tembo Abdul
(Chadema) aliyepata kura 416, Felista Yohana (CUF) 54, Mussa Kimonge
(SAU) 2, Mwandule Abdul (UDP) 2 na Ismail Ismail (Jahazi Asilia) ambaye
hakupata kura yoyote.
Mara - Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Nyasura, Mara, Simon Mayeye alimtangazaAlexander Mwikabe
wa CCM kuwa ameshinda baada ya kuzoa kura 966, akifuatiwa na Julius
Wassira (Chadema) kura 590, Asetic Matagira (NCCR-Mageuzi) 3, David
Waryoba (NLD) 1.
Iringa - Msimamizi
Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Nduli, Iringa Simba Nyunza alimtangaza
Basil Mtove wa CCM kuwa mshindi baada ya kuzoa kura 810 wakati Abdallah
Mwenda wa Chadema alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 491.
Tandahimba - Msimamizi
wa Uchaguzi Tandahimba wa Kata ya Mkwiti, Mtwara, Abdallah Njovu
alimtangaza Arafa Nakatanda (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 615
akifuatiwa na Abdallah Chiute wa CUF aliyepata kura 213 wakati Kawango
Mohamed wa Chadema alikuwa wa tatu kwa kura 76.
Dodoma - Msakati Hassan wa CCM aliibuka mshindi kwenye uchaguzi wa Kata ya Mirijo, Dodoma baada ya kupata kura 1,261.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Dk WilliamMaswere
alisema Bakari Saidi wa CUF alikuwa wa pili kwa kura 904 akifuatiwa na
Duka Salim (Chadema) kura 248, Juma Awadi (NCCR-Mageuzi) alipata kura
17.
Arusha - Mgombea
wa Chadema, Ally Bananga aliibuka mshindi Kata ya Sombetini, Arusha
baada ya kupata kura 2,564 . Mgombea wa CCM, David Mollel alipata kura
2,068 huku mgombea wa CUF Ally Mkali akipata kura 37.
Morogoro - Subiri
Mwandila wa CCM amechaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Rudewa, Kilosa-
Morogoro baada ya kupata kura 1,336 akiwashinda Evans Mwanisenga
(Chadema) aliyepata kura 698 na Yakwasi Mwasonganga (CUF) aliyepata kura
36.
Bagamoyo - Jarusu
Hamisi wa CCM aliibuka mshindi kwenye Uchaguzi wa Kata ya Magomeni,
Bagamoyo Pwani baada ya kupata kura 1,192. akifuatiwa na Mohamed Seif
(CUF) aliyepata 710 na Ligangwala Stanslaus (Chadema) 327.
Katika Kata ya Kibindu, Bagamoyo CCM kiliibuka kidedea baada ya kuzoa kura 1,213 dhidi ya 562 za Chadema.
Kilelema, Kigoma - Kiola
Norbet wa NCCR-Mageuzi aliibuka kidedea kwenye uchaguzi wa udiwani wa
Kata ya Kilelema, Buhigwe Kigoma kwa kupata kura 1,204 akifuatiwa na
William Abel (CCM) aliyepata kura 1050, Aaron Chisheko (Chadema) 449.
Chanzo - Mwananchi