Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Sunday, December 1, 2013

Kapuya atoswa

 
WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kukwepa kumkamata Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM) anayekabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi na kutishia kumuua, uongozi wa Bunge umeingilia kati ukitaka achukuliwe hatua.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimeibuka na kueleza kushangazwa na kitendo cha mbunge huyo kuikana namba yake ya simu 0784 993 930 wakati ipo hata kwenye kitabu cha wageni cha chama hicho alichokisaini mwenyewe mkoani Dodoma.
Prof. Kapuya ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne, tayari amefunguliwa jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam, tangu Novemba 24 mwaka huu.
Jalada hilo lilifunguliwa na mwanafunzi huyo anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa, lakini Jeshi la Polisi limekuwa likishughulikia suala hilo katika namna ya kumlinda mtuhumiwa.
Siku moja baada ya jalada hilo kufunguliwa, Kapuya alidaiwa kutimkia nchini Sweden, lakini taarifa za uhakika zinasema kuwa alirejea nchini Alhamisi na amekuwa akiishi kwa kujificha huku polisi wakidai kuendelea kumsaka.
Ni katika danadana hizo, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa suala hilo ni jinai na linapaswa liende katika mkondo wa kisheria.
 Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alikiri kulifahamu jambo hilo akisema kuwa walipomsikiliza mtoto huyo waliona ni suala ambalo linahitaji kushughulikiwa kisheria kwa kuwa ni jinai.
“Suala la binti huyo lilifikishwa kwangu kupitia msaidizi wangu ambaye alisikiliza hoja na rai yake na kushauriwa kuwa hilo ni suala la jinai na linapaswa liende katika mkondo huo.

“Hata hivyo, binti huyo alitambulishwa kwa spika kama kiongozi wa wabunge na kuelekeza kuwa tumshauri alifikishe katika mamlaka husika,” alisema Dk. Kashililah.
Chanzo chetu cha habari kilithibitisha kuwa binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali kabla ya viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikiri polisi kufungua jalada hilo na kuongeza kwamba hivi sasa wanafanya uchunguzi kubaini kama ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha unatoka katika simu ya mbunge huyo.
Lakini tangu kufunguliwa kwa jalada hilo, mtuhumiwa huyo ameendelea kubaki uraiani bila kuhojiwa, huku akiendelea kuwapa vitisho watoto hao, kusafiri nje ya nchi na kurejea kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere bila kukamatwa.
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hawana shamba mjini, kazi yao ni kukamata wahalifu na kuwa wangemsaka popote mtuhumiwa huyo ikiwa taarifa itafikishwa rasmi polisi.
Kwa siku tatu sasa jeshi hilo limekuwa likitupiana mpira kuhusu kumkamata na kumhoji mtuhumiwa huyo.
Wakati Kamanda Wambura akijitetea kuwa yuko mkoani Arusha, Kamishna Kova naye anadaiwa yupo nchini China, huku Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Isaya Mungulu akisema hadi jana alikuwa hana taarifa, hivyo kuomba muda zaidi ili leo aweze kutolea ufafanuzi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Mungulu alikuwa na taarifa tangu Kapuya anarejea nchini akitokea nje kwa ndege ya Shirika la Qatar ingawa yeye hakuwa tayari kufafanua suala hilo.
CCM wamuumbua
Kada wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dodoma ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, amemuumbua Prof. Kapuya akisema namba ya simu aliyoikana na kudai kuwa alishaigawa miezi sita iliyopita ndiyo hiyo aliiandika mwenyewe kwenye kitabu cha wageni.
Akiwa mjini Dodoma kama kamanda wa UVCCM, Kapuya alitembelea tawi moja na kusaini kitabu cha wageni ambapo mwisho wa saini yake aliandika namba hiyo ya simu ambayo pia imeandikwa kwenye kitabu cha orodha ya wabunge.
Kada huyo alisema kuwa alishitushwa kusikia Prof. Kapuya anaikana namba 0784 993 930 ambayo imekuwa ikiandikwa na gazeti hili kuwa ndiyo imekuwa ikitumika kutuma ujumbe wa vitisho kwa binti anayedaiwa kumbaka.
Alisema kuwa anampa ushauri wa bure Prof. Kapuya asijaribu kujiaibisha kwa kuikana namba hiyo kwa sababu hata kwenye moja ya vitabu vya wageni aliiandika na kusaini kwa mkono wake.
“25.6.2013 Alhaj Prof. Juma Athuman Kapuya, Mbunge wa Urambo Magharibi, Mjumbe wa NEC-CCM Taifa, Kamanda wa UVCCM (M) Tabora, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Juhudi zako zibarikiwe na Mungu 0784993930 CCM Oyee,” aliandika Kapuya katika kitabu kile.
chanzo:daima
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...