Rais wa Rottary Club Mzizima, Ambrose Nshala na Naibu Meya
wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge wakikata utepe kuzindua rasmi
mradi wa maji uliofadhiliwa na klabu hiyo katika shule ya msingi
Kumbukumbu Dar es Salaam jana.
Rais
wa Rottary Club Mzizima, Ambrose Nshala (kushoto), akijadiliana jambo
na Naibu Meya Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na Diwani wa Kata
ya Kinondoni, Husna Hemedi wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa kisima
cha maji uliofanyika Dar es Salaam jana.
………………………………………………………………..
Shule ya Msingi Kumbukumbu
iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni jana ilikabidhiwa mradi wa maji
safi ya kunywa wenye thamani ya zaidi ya Sh15Milioni uliotekelezwa na
Klabu ya Rottary Mzizima.
Akizungumza mara baada ya
kupokea mradi huo kutoka kwa Rais wa klabu hiyo, Ambrose Nshala katika
hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo jana, Naibu Meya wa Manispaa ya
Kinondoni Songoro Mnyonge alisema mradi huo una umuhimu wa pekee kwa
kuwa shule nyingi za Dar es Salaam hazina huduma za maji.
Alisema kutokana na hali hiyo
wanafunzi wengi wamekuwa wakienda shuleni na vidumu vya maji kwa ajili
ya matumizi ya vyooni kwa wanafunzi na hata walimu jambo ambalo
linahatarisha afya zao kwani maji ya namna hiyo ni machache na
yasiyokidhi mahitaji.
Songoro alisema mradi huo
umewapata changamoto kwao kutokana na ukweli kuwa kiasi cha fedha
kilichotumika ni kidogo kulinganisha na mradi wenyewe na kiwango hicho
kisingewezekana kwa miradi inayotekelezwa na manispaa na mradi kama huo
ungeweza kugharimu hadi Sh100 Milioni.
“Sheria ya manunuzi ni tatizo
kwani kwa mradi huu ungeambiwa si chini ya Sh100Milioni zimetumika na
hilo ni tatizo ambalo linakwamisha utekelezaji wa miradi mingi katika
manispaa” alisema na kuongeza kuwa kuna miradi mingi utekelezaji wake
umekwama kutokana na watalaam kuwasilisha bajeti zisizowezekana.
Awali akizungumza wakati wa
kukabidhi mradi huo, Rais wa Rottary, Ambrose Nshala alisema mradi huo
ambao unahusisha matenki ya maji ya lita zaidi ya 10,000 una mashine
pia ya kusafisha maji na kuyafanya yawe salama kwa kunywa kwa watoto
moja kwa moja kutoka bombani.
Alisema mradi huo ni fedha zao
wanachama na wahisani wengine na zingine zimetokana na mbio za hisani za
Rottary Marathon na shule hiyo ni moja kati ya zingine 25 za Jijini Dar
es Salaama ambazo zimesaidiwa kutatua kero mbalimbali na wahisani hao.



