Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Waziri Dkt. Fenella
Mukangara akizungumza na Viongozi wa Steps (hawako pichani) wakati
walipomtembelea ofisini kwake kwa mazungumzo juu ya maendeleo ya kazi za
sanaa jijini Dar es Salaam.
Mtaalam
Mshauri Bw. Sanctus Mtsimbe akichangia wakati wa kikao cha Steps na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella
Mukangara jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fissoo akichangia wakati wa kikao
kati ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt.
Fenella Mukangara na Steps.
…………………………………………………………………
Na Benedict Liwenga-MAELEZO
WAZIRI
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara
amekutana na wadau wa Kampuni ya Steps Entertainment na kuzungumza nao
juu ya maendeleo ya Tasnia ya Filamu nchini. Ujumbe huo wa Steps ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Dileshi Solanki.
Katika
mazungumzo hayo Dkt. Fenella amegusia masuala ya uharamia katika kazi
za filamu nchini na kutia mkazo katika suala zima la maadili. Aidha
Waziri ameeleza kuwa kuanza kwa urasimishwaji wa tasnia ya filamu na
muziki unaoendelea kutekelezwa nchini kutasaidia sana kuondosha kazi
zisizohalali.
Aidha,
Dkt. Fenella amewashauri wadau wa tasnia ya filamu nchini washirikiane
kikamilifu na Serikali katika kuendeleza na kukuza tasnia ya filamu na
pia kuhakikisha wasanii wananufaika na jasho lao. Aidha ameeleza umuhimu
wa kutoa elimu kwa wadau na umma kwa ujumla juu ya fursa nyingi
zilizopo katika tasnia.
Kwa
upande mwingine Waziri Dkt. Fenella ameshauri pia kuwe na majumba
maalum kwa ajili ya kuonyeshea sinema ambayo yatakuwa yanazipa
kipaumbele filamu za kitanzania pia amehamasisha wadau wa filamu
kuanzisha majumba hayo na ambao tayari wameanzisha kutoa fursa hiyo ili
kuziendeleza kazi za filamu za kitanzania.
“Kuwe na majumba ya kuonyeshea sinema ambayo yatakuwa yanazipa kipaumbele filamu za kitanzania”. Alisema Dkt. Fenella.
Kwa
upande wake Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo
alibainisha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la filamu zinazowasilishwa
kwa ukaguzi na pia wadau wameanza kutumia stempu za TRA katika kazi za
filamu na muziki ili kuzilinda kazi hizo.
Stampu zilianza kutolewa tangu
mwezi Januari mwaka huu .
Kwa
upande mwingine Mkurugenzi Mkuu Bw. Dileshi Solanki wa Kampuni ya Steps
Entertainment ameiahidi Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana na
Utamaduni na Michezo Mhe Dkt Mukangara, kuendelea kuendeleza tasnia ya
filamu kwa kushirikiana kikamilifu na serikali na kupiga vita uharamia
dhidi ya filamu za kitanzania . Aidha wameiomba serikali kuendelea
kuwajengea mazingira mazuri.





