
Mkuu wa wilaya ya Butiam,Angelina Mabula
Aina mpya ya ukatili wa kijinsia maarufu kama `memory card'
unaohusisha wanawake kuuawa na kunyofolewa sehemu za siri, imezua hofu
miongoni mwa wakazi wa wilaya Butiama mkoani Mara.
Kati ya kipindi cha Desemba mwaka jana na Julai, mwaka huu, jumla ya wanawake 14 wanasadikiwa kufanyiwa ukatili huo.
Ukatili huo umebainishwa na wanawake mbalimbali walipokuwa
wakizungumza kwenye mdahalo wa kupinga ukatili wa wanawake na watoto wa
kike uliofanyika katika kijiji cha Bisumwa, Wilaya ya Butiama mkoani
Mara ambapo walisema mauaji hayo yanaongozwa na kundi la watu wanaojiita
makhirikhiri.
Mdahalo huo ambao uliandaliwa na shirika la kutetea haki za wanawake
na watoto wa kike la Kivulini kupitia kampeni yake ya Tunaweza, wanawake
hao walisema ukatili huo umekuwa ukifanywa na watu walio karibu na
familia zao.
Kwa mujibu wa wanawake hao, katika kutekeleza ukatili huo, kundi hilo
la makhirikhiri huwavizia wanawake wanapokwenda kuteka maji au
wanapokuwa shambani na kuwavamia, kuwakata shingo na kisha kunyofoa
kiungo katika sehemu za siri.
Mmoja wa wanawake hao, Maria Michael, alisema wauaji hao huchukua
kiungo hicho pamoja na damu waliyokinga kutoka shingoni na kupeleka kwa
waganga wa kienyeji kwa ajili ya kutengenezewa dawa ya kupata utajiri.
“Mauaji ya wanawake na kukatwa sehemu zao za siri pamoja na kichwa
yamerudisha nyuma uchumi kutokana na wanawake hivi sasa kuhofia kutoka
majumbani mwao kwenda kushiriki kazi za kiuchumi,” alisema.
Aliongeza kwamba huo ni ukatili ambao unapaswa kukomeshwa mara moja
kwani hakuna uthibitisho wowote unaoonyesha kuwa kiungo hicho cha kike
kinaleta utajiri.
Kwa mujibu wa Maria, vitendo hivyo vya ukatili vimesababisha wanawake
kuungana katika makundi wanapokwenda kuteka maji au katika shughuli
nyingine za kiuchumi ili kuepuka kuvamiwa na kundi hilo la makhirikhiri.
Akitoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kukomesha mauaji hayo,
Elizabeth Samson, aliwataka viongozi wa serikali za mitaa kuacha urasimu
katika kushughulikia keso za ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kuwa polisi pia wamekuwa wakichelewa kushughulikia kesi za
ukatili wa kijinsia na baadhi yao hupokea rushwa na kuwaachia
watuhumiwa.
Akielezea hatua zilizochukuliwa ofisa wa sera na utetezi katika
shirika la Kivulini, Khadija Liganga, alisema mauaji hayo hufanyika kwa
siri na polisi walithibitisha kuyafuatilia kwa karibu ili kubaini maeneo
yanayoongoza.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula, alisema hivi
sasa matukio hayo yamedhibitiwa na serikali kwa kupitia kamati zake za
ulinzi na usalama za wilaya na mkoa pamoja na kuimarisha ulinzi
shirikishi.



