
Na Ali Issa-Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imetoa ruhusa ya kuendelea kwa ujenzi wa Jengo jipya la
Abiria katika Uwanja wa ndege wa Zanzibar lililosita kwa muda baada ya
kuonekana kasoro za kiufundi zilizojitokeza hapo awali katika jengo
hilo.
Hayo
yameelezwa leo huko Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa
Zanzibar na Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman
wakati alipokuwa akiwasilisha Bajeti yake ya Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya wizara hiyo.
Amesema
katika kutekeleza hilo ujenzi huo umeanza mara baada kukamilika kwa
taratibu za Michoro mipya kwa baadhi ya sehemu za jengo baada ya kupata
Mshauri elekezi kutoka Nchini Ufaransa.
“Mnamo
mwezi wa Machi mwaka huu tulimpata mshauri elekezi na kuaza kazi mwezi
April na kutoa ripoti yake mwezi juni mwaka huu ambavyo ilionesha namna
ya kasoro zilivyojitokeza na kuweza kutatuliwa haraka ipasavyo .”alisema
Waziri Rashid Seif.
Aidha
alifahamisha kuwa baada ya matokeo ya Ripoti hiyo mpya ya michoro
Serikali ilifuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na Benk ya Exim ya China
na kuwasilisha ombi la kuongezewa muda wa mkopo ambapo ungefikia
ukingoni tarehe 31 Julai mwaka huu.
Amesema
hali hiyo ilifanikiwa pamoja na kuiomba Serikali ya Mapinduzi pesa za
ziada ya mkopo ili kugharamia ongezeko linalotokana na kubadilika kwa
baadhi ya michoro ya jengo hilo na mazingira iliyo lizunguka .
Waziri
Rashid ameongeza kuwa ujenzi wa Uwanja huo unaendelea chini ya
Mkandarasi yule yule wa kampuni ya Beijing Construction Engineering
Group ya China chini ya usimamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Mshauri Muelekezi kutoka kampuni ya ADPI ya Ufaransa.
Kwa
upande wake Kamati ya Miundonbinu na Mawasiliano imependekeza kufanyiwa
Marekebisho Makubwa Barabara zilizochakaa katika maeneo ya Unguja na
Pemba.
Aidha
Wamependekeza Bandari ya Mkoani Pemba kupewa kipaumbele cha pekee kwa
kufanyiwa marekebisho ya haraka kutokana eneo lake kudidimia.
Wizara
ya Miundombinu na Mawasiliano imeliomba Baraza kuidhinisha jumla ya
shl. Bilioni 20.092 ili kuiwezesha Wizara hiyo kutekeleza majukumu yake
iliyojipangia kwa mwaka wa Fedha 2013/2014



