
Serikali
imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo
vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659
ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana. Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada. Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza
na mwandishi wetu jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo
walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
“Usajili
utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni, ‘Joining instructions’ (fomu ya
maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa wahusika kupitia anuani zao....
fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na mafunzo
ya Ufundi,” alisema.
Taarifa
ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa baadaye jana
ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kufika vyuoni wakiwa na
vyeti halisi vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa na Baraza la
Mitihani la Tanzania (Necta) , ada ya muhula wa kwanza Sh100,000 au
Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa
kuwa na “Sare ya chuo kulingana na maelekezo ya chuo husika, fedha za
tahadhari chuoni na matumizi binafsi,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi
wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye orodha iliyotolewa na wizara na si
vinginevyo.
Wengi
wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na
kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa kidato cha nne, matokeo
yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yalionyesha kuwa
watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la
nne.
Inaonyesha
pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, wanafunzi 34,599 walifaulu kwa
daraja la kwanza mpaka la tatu na kati yake waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa ni 34,213.
Kwa
upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa waliofaulu
mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao 40,242 wakiwa ni wa shule.
Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa 35,880 ndiyo waliofaulu
kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa
mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka 2012
wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya ualimu
nchini.
Kutokana
na takwimu hizo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wanaokwenda kusoma ngazi
ya cheti wanatoka kwenye kundi la wanafunzi waliopata daraja la nne.
Wanafunzi waliopata daraja la nne kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ni 124,260.
Baada
ya kutangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
tano pamoja na vyuo vya ufundi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi waliopata
daraja la nne katika kiwango cha alama 27 watachaguliwa kujiunga na vyuo
vya ualimu endapo wataomba.
“Vigezo
vya kujiunga na kidato cha tano na vile vya vyuo vya ualimu ni tofauti.
Kidato cha tano mwisho anatakiwa mtu mwenye alama 25 na masomo yake
matatu yawe sawa, ualimu ni alama 27.
“Mwanzoni
walikuwa wanakwenda wenye alama 28, lakini mwaka jana tukasema hapana,
iwe alama 27 na tutachukua kuanzia waliomaliza shule mwaka 2008 kama
wataomba, kwa sasa hivi watu wanaendelea na kazi ya kuwachagua,” alisema
Mulugo.
Kwa
muda mrefu, wadau wa elimu wamekuwa wakipiga kelele kuhusu wanafunzi
wanaochaguliwa kusomea ualimu nchini wakitaka nafasi hiyo ichukuliwe na
wale wanaofanya vizuri kwenye masomo yao.
Habari na Fredy Azzah
Chanzo - Mwananchi



