
Mwakilishi
wa mambo ya nje katika Muungano wa Ulaya Catherine Ashton amekutana na
Rais aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohammed Morsi katika eneo
lisilojulikana. Morsi amekuwa akizuiliwa na jeshi tangu kuondolewa
madarakani mapema mwezi huu.
Ashton
amewaambia waandishi wa habari mjini Cairo kwamba Bw. Morsi alikua
salama na kwamba alikubaliwa kutazama habari kwenye runinga na kusoma
gazeti.
Msemaji
wa Bi Catherene Ashton, alisema kuwa mkutano ulifanyika katika eneo
lisilojulikana ambako Morsi anazuiliwa na kuwa ulidumu kwa masaa
mawili.Alisema walijadili haja ya Misri kuganga yajayo na kuweka
amani.Baroness Ashton amesema mchakato wa utawala mpya sharti
ushirikishe pande zote
Hakutoa maelezo kuhusu walichokijadili.
Hata
hivyo tayari ameshakutana na maafisa kadhaa wa serikali akiwemo rais wa
muda Adly Mansour, mkuu wa majeshi, Generali Abdel-Fattah al-Sisi na
makamu wa rais wa maswala ya kigeni,Mohamed ElBaradei.
Alisema
kuwa atatoa wito kwa pande zote mbili kushirikishwa katika serikali.
Ziara ya Ashton ambayo ni ya pili nchini Misri inakuja baada ya wafuasi
zaidi ya sabini wa Morsi kuuawa kwenye makabiliano na vikosi vya usalama
nchini Misri.
Wafuasi
wa kiongozi huyo wamesema kuwa wanapanga kufanya maandamano Jumanne huku
serikali ya muda ikiwatahadharisha dhidi ya kuhusika na ghasia na kuwa
watakaovunja sheria watachukuliwa hatua.
Maafisa
wa usalama pia wametishia kuvunja maandamano ya wafuasi hao waliopiga
kambi nje ya medani iliyo karibu na msikiti wa Rabaa al-Adawiya mjini
Cairo.



