Afisa
Habari na Mawasiliano Bw. Munir Shemweta toka Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania Bw. Munir Shemweta juu ya faida za kuimarishwa kwa
mfumo wa sheria wa huduma za jamii kwa wazee utakaowezesha upatikanaji
wa huduma muhimu za maisha kwa kundi hilo ,wakati wa mkutano na
waandishi wa habari Jijini Dar Es salaam katikati ni Afisa Habari toka
Idara ya Habari Bw. Frank Mvungi na kulia ni Afisa Sheria Mkuu wa Tume
hiyo Bi. Anjela Shila.
Afisa
Sheria Mkuu toka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Anjela
Shila(kulia) akisisitiza jambo juu ya faida za kuimarishwa kwa mfumo wa
sheria wa huduma za jamii kwa wazee utakaowezesha upatikanaji wa huduma
muhimu za maisha kwa kundi hilo ,wakati wa mkutano na waandishi wa
habari Jijini Dar es Salaam.
Katibu
Msaidizi Elimu ya Sheria kwa Umma toka Tume ya Kurekebisha Sheria
Tanzania Bi. Agnes Mgeyekwa(kushoto) akitoa ufafafanuzi kuhusu namna
tume hiyo inavyotimiza majukumu yake katika kurekebisha sheria
mbalimbali nchini,wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar Es
salaam kulia ni Afisa Habari na Mawasiliano wa tume hiyo Bw. Munir
Shemweta.
……………….
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kupitia mfumo wa
sheria wa huduma za jamii kwa wazee (elderly social care) kwa nia ya
kubaini mapungufu yaliyoko kwenye mfumo huo na kutoa mapendekezo
stahiki ili kuweza kuwa na mfumo mzuri wa sheria utakaolenga ustawi na
hifadhi kwa wazee wote waliohitimu miaka 60 na zaidi wa mijini na
vijijini.
Wazee
wanapofikia umri mkubwa, uwezo wao wa kujihusisha na shughuli
mbalimbali hupungua na hivyo hushindwa kijihudumia mahitaji yao muhimu
ya kila siku kama vile chakula, mavazi, malazi, pamoja na kushiriki
katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa ziwe za kitamaduni,
kijamii au kiuchumi.
Tume
imeona kuna umuhimu wa kuimarisha mfumo wa sheria wa huduma za jamii
kwa wazee ili kuwezesha wao kupata huduma muhimu za maisha. Pamoja na
kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee (National Ageing Policy, 2003) Tanzania
haina sheria maalum katika eneo hili. Sheria mbalimbali za mafao
zinawagusa wazee wanaostaafu kazi serikalini na sekta binafsi ambao ni
sehemu ndogo sana ya kundi la wazee wengi wanaokosa huduma muhimu za
maisha.
Ikumbukwe
kuwa wazee hawa ni wale waliotumikia taifa kwa nguvu na moyo wote
kwenye ngazi mbalimbali wakati wakiwa na nguvu zao hivyo wanapokuwa
wamezeeka ni muhimu wakawekewa mfumo bora wa kisheria ili kuhakikisha
wanaishi maisha mazuri bila kujali kupungua kwa uwezo wao wa
kujishughulisha katika nyanja mbalimbali.
Kwa
sasa Tume inaendelea na rasimu ya awali ya kuangalia hali halisi ya
Tanzania kuhusiana na suala zima la wazee ikiwemo mikataba ya kimataifa,
mifumo ya kisheria na kijamii pamoja na sera na na baada ya hapo
itatembelea mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kwa nia ya kukusanya maoni
ya wananchi juu ya mfumo huo wa kisheria. Maoni hayo yatahusisha wazee
wenyewe, maofisa kazi, afya, ustawi wa jamii, watendaji wa vijiji,
taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojishughulisha na wazee pamoja na
wananchi kwa ujumla.
Ni
Matarajio ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuwa baada ya
kukamilika kwa mapitio ya mfumo huo wa kisheria kuhusiana na huduma za
jamii kwa wazee, Tume itakuja na mapendekezo ya kisheria na yasiyo ya
kisheria ambayo yataleta tija kwa taifa kwa ujumla.
Kuhusu Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
Tume
ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini
ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ilianzishwa kwa mujibu wa sheria
kupitia kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Namba 11
ya mwaka 1980. Sheria hii kwa sasa ni Sura ya 171 ya Sheria za
Tanzania kama sheria zilivyorekebishwa katika toleo la mwaka 2002.
Majukumu
ya Tume katika ujumla wake ni kutoa mapendekezo ya marekebisho ya
Sheria mbalimbali kwa Serikali, kwa kutafiti na kutathmini maeneo yote
ya sheria husika na kuyatolea mapendekezo kwa lengo la kuyaboresha.
Baada ya utafiti, Tume huwasilisha taarifa yake kwa Waziri anayehusika
na masuala ya sheria.
Moja
ya mafanikio ya Tume yaliyopatikana kutokana na mapendekezo ya Taarifa
zake zinazopelekwa kwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria ni pamoja
na kutungwa kwa sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
- Marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985 Kuhusu Kuwalipa Fidia Wahanga Wa Makosa Ya Jinai;
- Kuchapishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 192 la mwaka 1988 kuhusu Uharakishwaji wa Mashauri Mahakamani;
- Mapitio ya Sheria ya Udhibiti wa Ubadilishaji wa Fedha za Kigeni;
- Uanzishwaji wa Mfumo wa Wafungwa Kutumikia Sehemu ya Vifungo Nje ya Gereza;
- Marekebisho Makubwa Yalifanywa Kwenye Sheria 28 Kati ya 40 Zilizopendekezwa na Tume ya Nyalali Ikiwa ni Sehemu ya Mapendekezo Yaliyotolewa na Tume ya Kurekebisha Sheria Baada ya Kusoma Taarifa Hiyo ya Tume ya Nyalali
- Kutungwa kwa Sheria ya “Makosa ya Kujamiiana” Na. 4 ya 1998;’
- Marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai Ili Kutambua Utatuzi wa Migogoro kwa Njia za Usuluhishi;
- Kutungwa kwa Sheria za Kazi za Mwaka 2004;
- Kurekebishwa Sheria ya Ushahidi Ili Kutambua Ushahidi wa TEKNOHAMA (Electronic Evidence) Mwaka 2007;
- Kutungwa kwa Sheria ya Vinasaba vya BinadamuMwaka 2009;
- Kutungwa kwa Kanuni Mpya za Mahakama ya Rufaa (Court of Appeal Rules) za Mwaka 2009
- Kutungwa kwa Sheria Zinazohusu Haki za Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2009;na
- Kutungwa kwa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Imetolewa na:
Munir Shemweta
Afisa Habari na Mawasiliano
TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA
27 JULAI 2013






