WAZIRI MKUU MIZENGO KAYANDA PINDA.SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwataka polisi watembeze mkong’oto kwa watu wanaokaidi sheria na kanuni mbalimbali za nchi, wadau mbalimbali wamesema kiongozi huyo amepotoka na anapaswa kuomba radhi.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wadau hao walisema, Pinda amevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoapa kuilinda na kuitetea.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13(2) inasema: “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muun
gano wa Tanzania kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi ama wa dhahiri au taathira yake.”
Kifungu cha nne cha ibara hiyo hiyo kinasema: “Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi.” Pinda alitoa kauli hiyo akiwa anatekeleza kazi yake kama Kiongozi wa Serikali Bungeni.
Katiba Ibara ya 13 (6) (e) inaonya kuwa: “Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha, pia Ibara ya 16 ya Katiba inasema: “Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi ya nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na pia heshima na hifadhi ya maskani na mawasiliano yake binafsi.”



