Spika wa Bunge Anne Makinda juzi usiku alifunga mjadala wa
Bajeti Kuu ya Serikali, huku akiwaonya wabunge kwa kunukuu baadhi ya
vifungu vya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoashiria kuwa ikiwa
hawatopitisha bajeti hiyo Rais atalivunja Bunge.
Akiahirisha kikao cha 53 cha Mkutano wa 11 wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma juzi usiku, Spika Makinda alitaja Kanuni
ya 107 (1) na (2) ambayo hutumika kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2)(b)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Rais kulivunja
Bunge.
Kanuni hiyo ya 107.(1) inaeleza: “Mjadala kuhusu
Hotuba ya Bajeti ya Serikali utakapomalizika, Spika atalihoji Bunge ili
litoe uamuzi wake wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali ili
kukidhi matakwa ya Ibara ya 90(2) (b) ya Katiba.”
Akinukuu kifungu hicho cha Katiba, Makinda
alisema: “Rais hawezi kulivunja Bunge, isipokuwa kama Bunge litakataa
kupitisha bajeti.”
Mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka
2013/14 umejadiliwa kwa siku nne kuanzia Jumatatu wiki hii ambapo
Makinda alisema kuwa wote walioomba kuchangia walifanya hivyo
wamekwisha.




