Dodoma/Dar es Salaam. Huku
mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ukiwa unahitimishwa leo, wabunge wa
CCM wameshindwa kupata mwafaka wa kusimama pamoja ili kuipitisha.
Wabunge
hao walikutana jana jioni kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma kujadili
tofauti baina yao na kuwa na msimamo wa pamoja, lakini mgawanyiko wa
dhahiri ulionekana ndani ya kikao hicho baadhi wakipinga huku wengine
wakiunga mkono na kuwatisha wenzao.
Habari
za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema wabunge wengi wa chama
hicho walipinga bajeti hiyo wakiitaka Serikali kuzingatia mapendekezo ya
marekebisho waliyoyatoa wakati wakichangia mjadala. Mambo makubwa
mawili yaliyowagawa wabunge hao ni suala la kupandishwa kwa ushuru wa
petroli na hatua ya Serikali kupunguza asilimia moja tu kwa kodi ya
mshahara (PAYE).
Endelea kusoma habari hii kwa kufya hapa chini
Pia
wabunge hao waliitaka Serikali itekeleze mapendekezo ya marekebisho
yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew
Chenge.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama
alitumia muda mwingi kuwashawishi wabunge kuikubali bajeti hiyo.
Aliwaambia wabunge hao kuwa yeyote anayejiona hawezi kuunga mkono bajeti
hiyo ni bora asiingie kwenye kikao cha kesho (leo).
Habari
zaidi zinaeleza kuwa hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Sikonge,
Tabora, Saidi Nkumba aliyesema anayepinga bajeti hiyo, siyo tu asiingie
katika kikao hicho, bali atafute chama kingine.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema mbunge wa CCM atakayepinga ongezeko la kodi ya mafuta leo halitakii mema taifa.
Bajeti
iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa Juni 13, mwaka
huu ilipendekeza punguzo la asilimia moja la kodi hiyo, huku mafuta
yakiongezwa kodi kwa asilimia mbili kwa dizeli na petroli asilimia moja.
Mbunge
wa Geita, Dk Hamisi Kigwangalla ndiye pekee aliyepinga waziwazi bajeti
hiyo kwa upande wa CCM wakati wa mjadala akisema haina jibu kwa suala la
ajira kwa vijana, mfumuko wa bei, njaa, uhakika wa chakula na afya. Pia
alipinga ongezeko la kodi.
Licha
ya kuunga mkono bajeti hiyo, wabunge wengine wa CCM waliikosoa
wakibainisha kasoro kadhaa. Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba
alisema inawapa mzigo wafanyakazi kwa kuwapunguzia PAYE kidogo wakati
kwenye simu, mafuta (petroli na dizeli), vinywaji vyote kodi imeongezwa.
Mbunge
wa Kisesa, Luhanga Mpina na Kangi Lugola wa Mwibara kwa nyakati
tofauti, waliikosoa wakisema inamkandamiza Mtanzania wa kawaida. Bajeti
hiyo inayokadiriwa kufikia Sh18.2 trilioni imeelekeza nguvu zaidi katika
sekta za maji, nishati ya umeme, miundombinu ya barabara, ujenzi wa
bandari, reli, na elimu.
Bajeti
ya mwaka huu haikujadiliwa na wabunge wa Chadema kwani hawakuwapo kwa
takriban wiki nzima. Pia hakikusoma bajeti yake mbadala bungeni kutokana
na wabunge wake kwenda Arusha baada ya kutokea kwa mlipuko wa bomu Juni
15, kwenye Uwanja wa Soweto wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi
mdogo wa udiwani na kusababisha vifo vya watu wanne, kujeruhi zaidi ya
60.
Wabunge
hao wanarejea bungeni leo na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema,
John Mnyika alisema jana: “Hakubaliani na mapendekezo yote yenye
kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.”
Kauli
hiyo inapingana na ile ya Spika wa Bunge, Anne Makinda Alhamisi
akiwaonya wabunge kwamba ikiwa hawataipitisha Rais atalivunja Bunge.
Alitaja Kanuni ya 107 (1) na (2) ambayo hutumika kukidhi matakwa ya
Ibara ya 90 (2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inayohusu Rais kulivunja Bunge.
MWANANCHI