
Bunge jana
lilipitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambapo kwa
mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi nchini mwaka
1993, Bajeti hiyo ilipitishwa pasipo kwanza kusoma na kujadili Bajeti
mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Sio
nia yetu kujadili mazingira yaliyosababisha hali hiyo kwa sababu tayari
vyombo vya habari vimetoa taarifa za kutosha kuhusu tukio hilo. Hata
hivyo, yafaa tuseme hapa angalao kwa muhtasari tu kwamba wabunge wa
Chadema ambacho ndicho kinachoongoza kambi ya upinzani Bungeni walikuwa
jijini Arusha kuhudhuria mazishi ya watu waliokufa kutokana na bomu
lililorushwa wakati wa kufunga kampeni za udiwani za chama hicho.
Sisi
tunadhani kutosomwa kwa Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa
kisingizio kwamba wabunge wa Chadema hawakuwapo Bungeni ilikuwa ni
kasoro kubwa ambayo ilionyesha udhaifu katika uendeshaji wa Bunge la
Bajeti. Kanuni za Bunge zinaelekeza wazi kwamba maoni ya kambi hiyo
lazima yasomwe kabla bajeti ya kila wizara ya Serikali haijajadiliwa.
Hivyo,
Bajeti ya Serikali isingejadiliwa kabla kambi hiyo haijawasilisha maoni
yake. Tunadhani busara ingetumika kwa upande wa uongozi wa Bunge ili
kuepusha hali hiyo ya aibu kutokana na ukweli kwamba walioathirika na
kutosomwa kwa Bajeti hiyo sio wabunge wa Chadema au wa vyama vingine
kikiwamo CCM, bali wananchi wote kwa jumla ambao hawakuwa na namna
nyingine ya kujua nini kilikuwamo katika Bajeti mbadala ya kambi hiyo.
Tukizingatia
kasoro hiyo na nyingine nyingi zilizojitokeza tangu Bunge hilo la
Bajeti lilipoanza Mkutano wa 11 mjini Dodoma, tunalazimika kusema kwamba
Bunge hilo la Bajeti halikuwa na tija kwa Watanzania. Mbali na wabunge
wengi kuendeleza tabia za utoro na kuchapa usingizi, mijadala mingi
muhimu kuhusu bajeti za wizara ilitawaliwa na jazba za kisiasa badala ya
kujikita katika uzito wa hoja.
Kilichoangaliwa
zaidi ni mtoa hoja anatoka chama gani pasipo kutilia maanani umuhimu wa
hoja. Wabunge kadhaa, wakiwamo James Mbatia, John Mnyika, Zitto Kabwe
na Tundu Lissu walitoa hoja mbalimbali kuhusu masuala muhimu, lakini
hoja hizo ziliwekwa kando kwa sababu dhaifu. Kwa mara ya kwanza katika
historia ya Bunge, tulishuhudia baadhi ya wabunge kwa nyakati tofauti
wakiporomosha matusi ya nguoni ambayo hayatamkiki, huku kiti cha Spika
kikikaa kimya pasipo kuchukua hatua stahiki.
Pamoja na
Spika kuunda Kamati ya Bajeti chini ya Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge ili kuishauri Serikali kabla haijawasilisha Bajeti yake
Bungeni, Kamati hiyo haikupewa ushirikiano. Matokeo yake ni Bajeti
isiyokuwa na mwelekeo wala ubunifu, yenye vipaumbele vingi, vyanzo vipya
vya mapato vichache na ushuru na kodi zikiongezwa kwa bidhaa kama
petroli na dizeli zinazowagusa wananchi maskini moja kwa moja.
Ndio maana
mijadala mizito haikuelekezwa katika masuala nyeti ya kitaifa kama Deni
la Taifa linaloendelea kupaa, kilimo duni, ajira kwa vijana, kushuka kwa
elimu, mfumuko wa bei, mchango wa madini kwenye Bajeti na kadhalika.
Serikali ilipongezwa eti kwa kuwa sikivu kwa kufuta ushuru na kodi
kwenye bodaboda na bajaji. Bahati mbaya hawakujua kwamba waliosamehewa
kodi na ushuru sio vijana wanaoendesha vyombo hivyo, bali wamiliki wake
ambao ni matajiri.
Chanzo - Mwananchi



