
Bunge la Venezuela. |
Makonde
yameibuka bungeni na baadhi ya wabunge kujeruhiwa katika sintofahamu,
kutokana na mjadala kuhusu uchaguzi wa hivi karibuni unaobishaniwa.
Upande
wa upinzani ulisema juzi kwamba wabunge wao saba, walishambuliwa na
kujeruhiwa wakati wakipinga hatua ya kuwazuia kuzungumza katika Bunge
hilo, kutokana na kukataa kwao kutambua ushindi wa Rais Nicolas Maduro
uliofanyika Aprili 14.
Wabunge
wa chama tawala walilaumu wapinzani wao hao na kuwaita mafashisti kwa
kuanzisha vurugu, hali iliyoonesha siasa tete katika Taifa hili
mwanachama wa OPEC baada ya kifo cha Msoshalisti, Hugo Chavez mwezi
jana.
“Tulijua wapinzani wamekuja hapa kuanzisha ghasia,” Maduro alisema
kutokana na tukio hilo. “Hii haipaswi kujirudia.” Maduro (50), ambaye
aliteuliwa na Chavez kuwa mrithi wake, alimshinda mgombea wa upinzani
Henrique Capriles kwa asilimia 1.5 za alama. Capriles (40) amekataa
kutambua ushindi wake, akidai kuwapo kwa idadi kubwa ya upungufu na
kwamba kura ziliibwa. Uchaguzi huo ulibainisha mgawanyiko dhahiri wa
Taifa hili baada ya miaka 14 ya utawala wa kisoshalisti wa Chavez.
“Wanaweza kutupiga, kutufunga, kutuua, lakini hatutaweza kukiuka kanuni
zetu,” mmoja wa wabunge wa upinzani, Julio Borges, alikiambia kituo cha
televisheni, akionesha uso wenye michubuko na damu. “Masumbwi haya
yanatuongeza nguvu,” alisema.
Mfanyakazi wa Bunge, ambaye aliomba asitajwe jina, alisema tatizo
lilianza pale wabunge wa upinzani, walipopiga kelele za “fashisti” dhidi
ya kiongozi wa Bunge na kufunua bango la kupinga lenye maandishi ya
“mapinduzi ya Bunge”.
Wabunge wa chama tawala waliwashambulia. Kompyuta mpakato na meza,
vilitumiwa kushambuliana, huku mbunge mmoja akipigwa kichwani na kiti,
shuhuda alisema.
Baadaye wafanyakazi walilazimishwa kuonesha simu zao, kama zilikuwa na
picha au video kuhusu tukio hilo, mfanyakazi wa Bunge aliongeza.
Mbunge wa chama tawala, Odalis Monzon, alisema yeye na wenzake
walishambuliwa na kupigwa. “Leo tena nililazimika kulinda urithi wa
kamanda (Chavez),” alisema.
Vurugu hizo zilianza baada ya Bunge hilo linalodhibitiwa na serikali,
kupitisha hatua inayonyima upinzani haki ya kuzungumza bungeni hadi
umtambue Maduro kama rais.
“Mpaka watambue mamlaka, taasisi za Jamhuri, uamuzi wa watu wetu,
wabunge wa upinzani waende wakazungumze na vyombo vya habari vya binafsi
na si hapa bungeni,” alisema Diosdado Cabello, ambaye ni Spika wa
Bunge.
Pande zote mbili zilianza kushutumiana faragha bila waandishi wa habari
kuwapo. Video zilizopatikana na kituo cha televisheni chenye ufuasi wa
upinzani cha Globovision kutoka kwa mmoja wa wabunge, zilionesha wabunge
hao wakipigana huku wengine wakipaza sauti za kuwazuia.
Venezuela imekuwa katika mgogoro tangu uchaguzi wa Aprili 14. Takribani
watu wanane walikufa katika maandamano siku mmoja baada ya uchaguzi.
Kumekuwa na kamatakamata ambayo wapinzani wanaiita wimbi la
ukandamizaji.
Maduro ametuhumu upinzani kwa kupanga mapinduzi. Mtawala wa zamani wa
Taifa hili, Hispania, wiki hii alitoa mwito wa kufanyika mazungumzo ya
kuondoa mvutano wa kisiasa nchini. Lakini, Maduro alikataa.
“Acheni
kuingiza pua zenu Venezuela. Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania, ondoka,
wewe fidhuli. Venezuela lazima iheshimiwe,” alisema Maduro katika
hotuba yake akimaanisha Waziri wa Mambo ya Nje, Jose Manuel
Garcia-Margallo.