Diwani wa Kata ya Kitanzini Manispaa ya Iringa Mjini, Jesca
Msambatavangu(wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vyo shiriki
vya mashindano ya Pool yanayotarajiwa kuanza kesho Mkoa wa Iringa.Kushoto ni
Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania(TBL) Mkoa wa Iringa, Josephat Changwe.Kutoka
kulia ni Katibu wa chama cha pool Mkoa wa Iringa,Haji Kiyeyeu na Mwenyekiti wa
chama hicho,Salum Kisaku.
Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania(TBL) Mkoa wa Iringa,
Josephat Changwe (kushoto) akimkabidhi tisheti Diwani wa Kata ya Kitanzini
Manispaa ya Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu ili awakabidhi vyuo shirika vya
elimu ya juu kwenye mashindano ya Pool kwa vyuo hivyo Iringa jana.Kulia ni
Mwenyekiti wa chama cha Pool Mkoa wa Iringa Salum Kisaku.
Na Mwandishi Wetu,Iringa
VYAMA vya mchezo wa pool kuanzia wilaya hadi taifa vimetakiwa kutumia
vizuri udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuhakikisha mchezo huo
unaenea katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Hayo yalisemwa jana na diwani wa kata ya Kitanzini katika Manispaa ya
Iringa, Jesca Msambatavangu wakati alipokuwa mgeni rasmi wakati wa
kukabidhi vifaa vya michezo kwa vyuo vikuu vitakavyoshiriki mashindano
ya mchezo huo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ngazi ya mkoa wa Iringa ya
'Higher Learning Pool Competition 2013'.
Msambatavangu alisema kuwa ni vema vyama vya mchezo huo vikatumia nafasi
ya udhamini huo vizuri katika kuhakikisha mchezo wa pool unapanuka
zaidi ili hatimaye uchezwe kila mkoa kwa mikoa yote ya Tanzania Bara
kuanzia kwenye klabu na vyuo vikuu.
"Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru na kuwapongeza TBL
kupitia bia ya Safari Lager kwa kuutoa mbali mchezo wa pool na hatimaye
kuufikisha hapa ulipo na pia udhamini wa kampuni yenu si katika mchezo
wa pool pekee bali ni mambo mengi mnayoyafanya kwenye jamii katika
kuchangia maendeleo ya taifa letu na serikali inalitambua hilo,"alisema
Msambatavangu.
Aliongeza kwa kuwataka vijana wengi kuendelea kujitokeza kujifunza
kucheza mchezo huo ambao kwa sasa ni ajira kwa vijana wanaoucheza.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni mmoja wa wadau wa mchezo huo, diwani
huyo aliahidi kutoa mbuzi mmoja mmoja kwa kila chuo kinachoshiriki
mashindano hayo.
Naye mwenyekiti wa chama cha mchezo huo mkoa wa Iringa (IRPA), Salim
Kisaku alisema kuwa mashindano hayo yatakayoshirikisha vyuo vikuu vinne
yatafanyika kesho kwenye ukumbi wa Twisters Club.
Kisaku alivitaja vyuo vitakavyoshiriki mashindano hayo kuwa ni Ruaha, CDTI, Mkwawa na Tumaini.
Alisema kuwa chuo kitakachobeba ubingwa wa mkoa huo ndiyo
kitakachoushirikisha katika fainali za taifa za mashindano hayo
zitakazofanyika juni mosi jijini Dar es salaam.
Meneja wa Kampuni ya TBL mkoani hapa, Josephat Changwe alisema kuwa
bingwa wa mashindano hayo kwa upande wa timu katika mkoa huo
atajinyakulia fedha taslim Sh.500,000, mshindi wa pili Sh.300,000,
mshindi wa tatu Sh.200,000 na mshindi wa nne Sh.100,000.
Changwe alisema kuwa kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) bingwa
atazawadiwa Sh.150,000 na mshindi wa pili Sh.100,000 wakati kwa upande
wa wanawake bingwa atapewa Sh.100,000 na mshindi wa pili Sh.50,000.
Diwani wa Kata ya Kitanzini Manispaa ya Iringa Mjini, Jesca
Msambatavangu (kushoto) akimkabidhi tisheti nahodha wa timu ya chuo Kikuu cha
Ruaha, Said Mohamed wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa
vyuo shiriki vya mashindano ya Pool kwa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoa wa
Iringa.Katikati Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Pool Mkoa wa Iringa,Salumu
Kisaku na Katibu wa chama hicho,Haji Kiyeyeu.