Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa CUF.
Chama
Cha Wananchi (CUF) kimesikitishwa sana na vurugu zilizotokea Mtwara
tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na
polisi tarehe 23 Mei 2013. Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi
na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za
miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa
ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi
na Ruvuma katika gridi ya taifa.
CUF
inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea nyumba ya mwandishi
wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, na
nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani vikali vitendo
vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la Mikindani
linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
CUF
imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari wanne wa JWTZ kwa
ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa
toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.Tumepeleka
salamu za pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia
za marehemu. Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa
Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa
letu.
Vilevile
tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa kupigwa risasi akiwemo mama
mjamzito na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole familia za marehemu na
kuwaombea wote waloumia wapone haraka na waendelee na shughuli zao.
Taarifa
za vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia hizi zilianza baada ya
hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa katika Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi wa bomba la
kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Taarifa
tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia asubuhi, wakati
Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali bungeni kwa niaba ya Waziri
Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa Jeshi la Polisi
walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia.
Polisi
walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na
kuwachukua kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za
moto zilipigwa hovyo hovyo.
Aidha
katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo waliwapiga wake zao, watoto
wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao wanasumbua. Binti
mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. Katika eneo la Mkana
Read, Polisi walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za raia
zimechomwa moto na polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya
wafanyabiashara. Wananchi wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia
nyumba zao. Taarifa tulizopata zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi
vilisita baada ya maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi kufika Mtwara.
Vurugu
zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi Jeshi la Polisi kupiga
watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara na kupora mali
za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali na kuchoma
vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana.
Weledi
ndani ya Jeshi la Polisi uko chini sana. Tunalaani vikali vitendo vya
Jeshi la Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na kupora. Uongozi wa
Jeshi la Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya polisi
waliohusika na vitendo hivyo. Tunatoa wito kwa asasi za haki za binadamu
na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai haki
zao.
Pamoja
na kulaani vitendo hivi vya kihalifu na kuchukua hatua za kisheria
dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo, Serikali itafanya makosa
makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu na wananchi wa
mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na
kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa
wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu.
Narudia
Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa
kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya
Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua
umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya
taifa.
Mradi
mwingine ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama
malighafi kama ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki
visima vya gesi ya Mnazi Bay na Msimbati. Kama miradi hii ingeanza
kutekelezwa nina uhakika wananchi wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga
gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.
Kauli
ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali itawasaka waasisi wa vurugu
hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta mchawi badala ya
kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa serikali ya
CCM. Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata viongozi
mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea,
kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF.
Serikali
ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu wasiokuwa na hatia.
CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi tumejenga hoja
za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu utekelezaji
wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza. Viongozi wa
CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara na
maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.
Mimi
binafsi nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa kufanya mkutano wa
hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya ya
Tandahimba. Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja na
kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali.
Tarehe 14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa
hadhara sikukaidi nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu
wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya
mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa
wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.
Kuwakamata
viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa kitaifa hakutamaliza
mgogoro kati ya serikali na wananchi wa Mtwara ikiwa serikali
itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza. Badala yake itaongeza
chuki dhidi ya serikali.
Wakati
wananchi wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi wa CCM na serikali
yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za kiraia
kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo
kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia. Umma uliokata tamaa na
unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza
kuchukua hatua zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.
Serikali
imekuwa inapotosha kwa makusudi madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara
ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi ya gesi iliyoahidi wananchi wa
Mtwara. Badala yake wananchi wa mikoa mingine wanalishwa sumu kuwa
Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi iwanufaishe Watanzania
wengine. Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa katika gridi ya taifa
utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi ya taifa. Kiwanda cha mbolea
cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi nzima. Wananchi wa
Mtwara hawajasema Watanzania wengine hawana haki ya kwenda Mtwara kupata
ajira au kufanya shughuli za kibiashara.
Wanaobomoa
umoja na mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza, kuwadharau na
kuendelea kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza sumu kwa
Watanzania wengine kwa kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara
na kushindwa kwa serikali kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi
akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.
Wananchi
wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na kupeleka ombi (petition)
kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kujadili kutekelezwa kwa
miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia ombi hilo
kujadiliwa.
Bunge
limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa nini mradi wa kufua umeme
MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12 ulitengewa na kutumia
shilingi 540 milioni umesitishwa. Mpaka hivi sasa hakuna kamati ya Bunge
iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake Spika
amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya
kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.
Katika
hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza serikali kupitia TANESCO
kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga kituo cha kufua
umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea.
Hata
hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu wala kutenga hata
shilingi 1 kwenye mradi. Wananchi wa Mtwara wanaona wanaendelea
kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli za kejeli za
Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara katika
masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi.
Mpaka
hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba na
upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati
haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya gesi wataweza
kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara
kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia gesi mkoani
Mtwara.
Linalonistusha
na kunitisha ni kwa nini viongozi wa juu wa serikali hawataki kuwa
wawazi kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha, kuwagawa wananchi na
kudanganya alimuradi mradi huu utekelezwe na usihojiwe?
Gesi
ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982 lakini mpaka hivi
sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza utaratibu wa
kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18. Tarehe
17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake wa
kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa
kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi - Netherlands
Development Finance Company. Gharama za mradi wa kufua umeme
zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225.
Kampuni
maalum ya kuendesha mradi huu ya Tanzania Generation Company Ltd
(TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na kuendesha mradi huu. Kampuni hii
ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65 zingechangiwa kama hisa na
kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya
madini ya Barrick International.
Kampuni
nyingine maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili ijenge msongo wa umeme
(nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na kuunganisha umeme wa Mnazi Bay
kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu dola milioni 400. Mradi huu
ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania na wawekezaji
kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na
ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme
(National Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW
300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco
inaueleza mpango huu kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali
iliukabali mradi huu baada ya kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.
Mtikisiko
wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008 uliathiri kampuni ya
Artumas. Thamani ya hisa moja ya Artumas iliporomoka toka dola za
Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia dola 0.12 mwezi wa Machi
2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata na ilibidi serikali
iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na ufuaji wa umeme wa MW 18
Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa TANGEN. Katika
kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina
lake na kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.
Tarehe
10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa anawahutubia Wabunge na Wananchi
katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari za mtikisiko wa uchumi
duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega
uchumi kutoka nje umepungua.
Wawekezaji
wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo
yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo
ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira. Kwa mfano:
Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd.
kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel
Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme
mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.”
Kwa
kauli ya Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla
waliisikia kwani hotuba hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji la
Tanzania – Radio na Televisheni na vyombo vingine vya habari.
Miradi
ya kutumia gesi ni pamoja na kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea
inayotumia gesi kama malighafi, aluminium smelter inayohitaji umeme
mwingi, na kiwanda cha saruji ambacho kinatumia umeme na kinu chake
kinaweza kutumia gesi. Wananchi wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa
miradi hii imekwama kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali
inajitahidi kutafuta njia mbadala ya kujikwamua ili miradi hiyo
iendelee.
Wakati
wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete aliwaeleza wananchi wa
Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara itakayotumia gesi ya
Mnazi Bay. Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010, ibara ya 63
kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi Bay
(k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi
kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.
Mitambo
ya kufua umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa itumie gesi ya Songosongo
kwani bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka Dar es Salaam
lingepanuliwa. Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas ilijiandaa
kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka Songosongo –
Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya kufua
umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. Serikali iliisitisha
kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa
umekamilika na kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau
MW 200.
Rais
Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya Mashujaa tarehe 25 Julai
2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza miradi ya maendeleo
itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo ufuaji wa umeme
wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.
Tarehe
12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa “Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili
ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao
utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko
kwenye gridi hiyo. Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni
ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation
(CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia
kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo
la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya
kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huo mkubwa wa umeme wa
megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na
utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300
kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo
kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”
Mikoa
sita ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa ni Lindi, Mtwara,
Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na kufua umeme wa MW
300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye gridi
ya taifa. Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa yote ya
Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa
na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa
kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa
imetimimiza ahadi hiyo.”
Maelezo
haya yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari vikayatangaza na wananchi
wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme kutaifanya Mtwara
iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni kuanzisha viwanda hasa
ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya Mtwara. Mwaka wa
fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi 540 milioni
fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development Project.
Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena. Badala ya mradi huu
kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa
ujumla badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa kujenga bomba
la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Kwa
taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme wa MW 300 Mtwara na
kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa gharama yake ni dola
milioni 684. Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa na mkopo wa
dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China. Ni wazi
gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye gridi ya
taifa ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.
Msongo
wa umeme za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa – Dodoma – Singida na
Shinyanga. Mradi huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga umeme za kV 400 ni dola
za Marekani 600,000 kwa kilomita 1. Gharama za kujenga bomba la gesi
lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa kilomita 1. Kwa
madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni zaidi ya
mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam. Isitoshe
unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusamabaza kwa msongo huo
huo.
Ujenzi
wa bomba la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya
kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es
Salaam. Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo
bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa ni
futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za
ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.
Mpaka
hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33.7 imegunduliwa
katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza.
Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi
kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado hazijafanya uamuzi
wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi nchi kavu. Kwa kuwa
gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni za juu sana,
kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu kwenye eneo
lililo fupi kuliko yote.
Statoil
imegundua gesi nyingi eneo la Zafarani bahari kuu eneo la mkoa wa
Lindi. Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa kuweza kuweka kituo cha nchi
kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa ambayo ina
kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. Kwa hivi sasa hakuna uhakika
gesi iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga
bomba kubwa umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida
zake kiuchumi. Jambo la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na
kuacha kutekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi,
kijamii na uwajibikaji wa kisiasa?
Wentworth
Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini
kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza
kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza
mbolea na kemikali nyingine Mtwara. Kiwanda cha mbolea chenye faida
kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya gesi
iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay. Mradi wa kujenga
kiwanda unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea kiwanda
kitazalisha methanol yenye soko kubwa duniani. Kiwanda kitatumia hewa
ukaa (carbondioxide) na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha
mazingira. Uongozi wa Wentworth Resources una uzoefu wa miaka mingi
katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza. Hata hivyo
serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi
la kwenda Dar es Salaam.
Serikali
imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa
kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi yenye manufaa makubwa
kiuchumi na kijamii kwa taifa letu. Uchunguzi huru na wa kina ufanyike
kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara na
kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa
kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa itolewe
ili Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu. Mkataba wa mkopo na
utekelezaji wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi. Serikali
iruhusu kampuni ya Wentworth resources kuendelea na mradi wa kiwanda cha
mbolea. Rais aende Mtwara kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza za
kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.
Vyama
vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara
kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za wananchi wa
Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa nini Mradi wa Kufua
umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa
bomba la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.
Sakata
hili la gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa hatuna sera muafaka na
mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa letu na
Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa itakuwa
balaa na laana. Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu zitakazohakikisha
kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na utakaolinufaisha
taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye teknolojia ya
kutafuta na kuchimba gesi. Wananchi wa Mtwara wanahitaji kushirikishwa.
Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi ya gesi.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba