MHINDI
mwenye uraia wa India, Srinivasa Rao Talluri, 36 anayedaiwa kumuua
Mwalimu Elizabeth Mmbaga wa Shule ya Msingi Atlas, jijini Dar es Salaam
amejiua Aprili 17 mwaka huu katika Hoteli yaTransit iliyopo Karakata.
Talluri
ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya vinywaji vikali
ijulikanayo kwa jina la Moan’s Drinks Ltd iliyopo Oysterbay, Dar maiti
yake ilikutwa chumbani saa mbili asubuhi na inadaiwa alijiua kwa kunywa
sumu ambayo mabaki yake yamepelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa
uchunguzi. Habari za kipolisi zimesema kuwa baada ya wafanyakazi wa
Hoteli ya Transit jijini Dar kugundua kuwa Mhindi huyo amekufa, walitoa
taarifa polisi ambao walifika na walipochunguza chumbani, walikuta kuna
pombe aina ya Pushkin chupa tatu, chupa yenye sumu ya kuulia wadudu,
chips na maziwa glasi moja.
Inadaiwa
kwamba Mhindi huyo aliachishwa kazi katika kampuni hiyo Aprili 2, mwaka
huu baada ya kugundulika kuwa alitumia vibaya zaidi ya shilingi 400,000
ambapo Aprili 3, mwaka huu alifikishwa polisi Kituo cha Oysterbay,
jijini Dar. Mwandishi wetu alifika katika ofisi za Moan’s Drinks Ltd
alikokuwa akifanyia kazi Mhindi huyo na kuonana na mmoja wa viongozi wa
kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Raju na akakiri kutokea
kwa kifo cha Talluri. Habari zinasema mwili wake ulifanyiwa uchunguzi
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jumatatu iliyopita na
ukasafirishwa kupelekwa India Jumatano ya wiki iliyopita kwa ajili ya
mazishi.
CREDIT-joycekiria.com