Watu wasiopungua wanane wameuawa katika mapambano kati ya jeshi la
Algeria na watu wenye silaha waliokuwa wakijaribu kujipenyeza nchini
humo kupitia mpaka wa nchi hiyo na Libya.
Ndege ya upelelezi iligundua msafara wa magari manne yaliyokuwa
na watu wenye silaha kujaribu kuingia Algeria kwa kuvuka mto katika eneo
la mpakani.
Mapambano hayo yalisababisha vifo vya watu watano wenye
silaha na wanajeshi watatu. Jeshi la Algeria linawasaka watu wengine
kumi, na kusema wengi wao ni Waalgeria na baadhi ni Watunisia.
Hii ni operesheni kubwa kufanyika na jeshi la Algeria toka
shambulizi la kigaidi lililotokea Januari wakati kisima cha kuchimba
gesi cha Tiguentourine mkoani Illizi nchini humo kushambuliwa na
kusababisha vifo vya wafanyakazi 37 wa nchi za nje pamoja na mwalgeria
mmoja.




