Wakati vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vikiendelea
kushika kasi nchini, mwanasaikolojia ameeleza kwamba vinachangiwa na
hasira za muda mrefu kiasi cha kuwafanya watu kukata tamaa.
Aidha, mwanasaikolojia huyo, Dk. Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, ameeleza pia kwamba kukata tamaa huko (frustration) kunachangiwa
na hali ya wananchi kutonufaika na rasilimali za nchi yao kwa kipindi
kirefu.
Alisema hasira za muda mrefu kwa wananchi dhidi ya vyombo vya dola
hususani Jeshi la Polisi pamoja na uvunaji wa rasilimali usiowanufaisha,
unachangia 'uasi' wa wananchi unaosababisha kujichukulia sheria
mkononi.
“Kila tukio (la kujichukulia sheria mkononi), lina maana yake.
Ukiangalia kule Liwale ni korosho, Loliondo ni ardhi, Mtwara ni gesi,
mauaji ya polisi kama kule Ngara na Rufiji ni hasira dhidi ya
kutotendewa haki na vyombo vya dola na yote hii ni hasira za muda
mrefu,” alisema.
Alisema kwenye maeneo kama Mtwara au Liwale, wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa
kuwa wameona hawanufaiki na rasilimali zinazowazunguka.
Dk. Mkumbo alisema hasira hizo zinaibuka zaidi kwa sababu wananchi
wanahangaika kujitafutia ajira kama usafiri wa boda boda, lakini katika
hali ya kushangaza vyombo vya dola vinachangia kuminya ajira hizo, jambo
linaloamsha hasira.
“Kwamba ajira hakuna, halafu watu wamehangaika hadi wamejiajiri au
wamelima, lakini bei waliyoahidiwa hawaipati kwa hiyo wanaona njia pekee
ni kupambana na wale wanaozuia malengo au mafanikio yao,” alisema.
Dk. Mkumbo alisema ili kumaliza hali hiyo, ni lazima wenye mamlaka watimize wajibu wao kikamilifu.
Kauli hiyo ya Dk. Kitila Mkumbo inakuja wakati ambao matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamekithiri nchini.
Katika matukio ya hivi karibuni, ni lile la mwishoni mwa mwaka jana
lililosababisha askari wawili wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara Mkoani
Kagera, kuuawa na wananchi wenye hasira kali.
Mauaji hayo yalifanyika baada ya wananchi hao kuvamia na kukichoma moto
kituo cha polisi cha Mugoma wilayani humo kufuatia askari hao kudaiwa
kumpiga risasi fundi wa pikipiki.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea mchana wakati askari
kadhaa wa kitengo cha usalama barabarani walipofika kwa fundi pikipiki
huyo na kutaka kuichukua pikipiki aliyokuwa akiitengeneza kwa madai kuwa
ilikuwa na makosa.
Habari zilisema kuwa fundi huyo aligoma na kueleza kuwa asubiriwe mwenye pikipiki ili kuepuka kudaiwa chombo hicho cha usafiri.
Baada ya mvutano wa muda mfupi, askari hao walifyatua risasi na kumpiga
fundi huyo mguuni na kifuani, hivyo kusababisha kifo chake.
Tukio hilo liliwapandisha hasira wananchi na kuwafukuza askari hao
waliokimbilia katika kituo hicho cha polisi na ndipo waliamua kukichoma
moto hatua iliyosababisha askari waliokuwamo kutoka na kukimbia kila
mmoja na muelekeo wake.
Hata hivyo, Koplo Paschal alianguka wakati akijinusuru, hivyo kuvamiwa
na wananchi waliokuwa na zana mbalimbali za jadi ambazo walizitumia
kumshambulia na kumuua papo hapo.
Wananchi hao pia wanadaiwa kumfuata askari mwingine anayetajwa kwa jina
la PC Alex aliyekuwa amekimbilia kwenye nyumba ya mwananchi mmoja na
kumtoa kwa nguvu na kisha kuanza kumshambulia hadi kumuua.
Katika tukio hilo, nyaraka mbalimbali ziliteketea vikiwamo vizibiti kama pikipiki na baiskeli zilizokuwa kituoni hapo.
Mapema mwezi huu, raia walivamia kituo cha polisi Kawe jijini Dar es
Salaam na kuharibu mali pamoja na nyaraka kituoni hapo baada ya watu
wanasadikiwa kuwa ni wanajeshi waliotuhumiwa kumuua dereva wa bajaji,
Yohana Cyprian kupelekwa kituoni hapo.
Tukio hilo lilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya
wananchi waliokuwa wakishinikiza polisi wamwachie mtuhumiwa ili wamuue.
Katika tukio hilo, watu 12 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
MTWARA
Tukio la Kawe lilitokea wiki kadhaa baada ya polisi mkoani Mtwara
kulazimika kupiga mabomu ya machozi kutwa nzima katika kata ya
Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani kutawanya wananchi
walioizingira nyumba ya diwani wa kata hiyo, Mohamedi Chehako, kwa madai
ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.
Wananchi hao waliokuwa na hasira walichoma moto Mahakama ya Mwanzo na
kuvunja vioo vya nyumba za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Hawa Ghasia na ya Mohamed Said Sinani ambaye ni Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mtwara.
Wakiwa katika mahakama ya mwanzo, polisi walizingirwa na vijana
waliokuwa wamebeba mawe na kufunga barabara zote za kuingia na kutoka
Kituo Kikuu cha Mabasi na eneo la Soko Kuu, licha ya kufyatua hewani
mabomu ya machozi.
Hayo yalitokea huku mkoa wa Mtwara ukiwa umeshuhudia maandamano na
mapigano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, kutokana na msimamo wa
wananchi kupinga uamuzi wa serikali wa kutaka kuisafirisha gesi asilia
kutoka mkoani humo na kuipeleka Dar es Salaam kwa njia ya mabomba.
DUMILA
Tukio la Mtwara lilitokea siku ambayo vurugu kubwa zilikuwa zimezuka
katika eneo la Dumila mkoani Morogoro baada ya wananchi kuchoma moto
nyumba na kupasua vioo vya magari na hivyo kuzuia magari yote
yanayotumia barabara hiyo, kwa madai kuwa wanapinga agizo la Mkuu wa
Wilaya hiyo la kuwanyang'anya ardhi wakulima na badala yake kupewa
wafugaji.
Vurugu hizo zilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.
KIBITI
Tukio lingine ni lile la wananchi wenye hasira kuvamia kituo cha Polisi
Kibiti Wilayani Rufiji na kuleta vurugu kubwa kufuatia raia mmoja kufa
kwa kile kilichodaiwa kipigo cha polisi.
Vurugu hizo zilitokea baada ya kijana Hamis Mpondi aliyedaiwa kupigwa na
polisi kufariki wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili.
Wananchi hao waliteketeza nyumba za askari polisi hao zilizopo jirani na
kituo hicho, licha ya juhudi za polisi kuwatawanya kwa mabomu.
Aidha, wananchi hao walifunga barabara kuu ya Kilwa iendayo mikoa ya
Kusini, Lindi na Mtwara kwa mawe, magogo na kuchoma matairi umbali wa
kama kilometa moja kutoka kituo cha Polisi Kibiti.
MWANZA
Tukio jingine ni lile la mkoani Mwanza, ambako Polisi walazimika kutumia
risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waendesha bodaboda
waliokuwa wakiwalazimisha askari wawaachie wenzao waliowakamata kwa
makosa mbalimbali.
Ghasia hizo ziliibuka wakati polisi wa usalama barabarani na kikosi
maalumu cha ukaguzi wa magari walipofanya doria kukagua leseni na
uhalali wa madereva hao wanaofanya shughuli za kusafirisha abiria.
Vurugu hizo zilianza baada ya polisi kuwakamata waendesha bodaboda
wapatao 26, ambao walitozwa faini za papo kwa papo kulingana na makosa
yao, huku wengine wakiendelea kushikiliwa.
Hatua hiyo iliwafanya waanze kujikusanya kutoka sehemu mbalimbali na
kuandamana hadi eneo kulikokuwa limetengwa kwa ukaguzi huo katika mtaa
wa Mission.
Baada ya kufika eneo hilo, walianza kuwarushia mawe askari hao, huku
baadhi yao wakiendesha pikipiki kuzunguka eneo hilo na kuzuia magari
kupita hali iliyozua tafrani.
Baada ya kutokea hivyo, askari hao walilazimika kuwaita askari wengine ili kuwakabili vijana hao.
Vurugu hizo zilizodumu kwa saa tatu, zilisababisha kufungwa kwa barabara
iendayo Uwanja wa Ndege na katika eneo la Pasiansi, huku baadhi ya
abiria wakilazimika kuteremka katika daladala na kukimbia ovyo na
wengine kulala katika mifereji ya maji machafu baada ya milio ya risasi
na mabomu ya machozi kuanza kurindima.
chanzo:nipashe
(3)(6).jpg)



