THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta
kuomboleza kifo cha Mjumbe wa Baraza la Seneti na Waziri muhimu wa
zamani wa nchi hiyo, Mheshimiwa Mutula Kilonzo, aliyefariki dunia juzi,
Ijumaa, mjini Nairobi.
Katika
salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amemwambia Rais Kenyatta kuwa
amepokea habari za kifo cha ghafla cha mwanasiasa huyo kwa mshtuko na
huzuni na kuwa kifo chake kimeipokonya nchi hiyo mmoja wa viongozi
waliokuwa wanajali na kutanguliza maslahi ya Kenya na wananchi wake.
“Kwa
hakika, kifo cha Mheshimiwa Mutula Kilonzo kimeipokonya Kenya kiongozi
muhimu. Mchango mkubwa aliuotoa katika kipindi cha kuivusha Kenya kutoka
kwenye changamoto za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 hadi sasa ambako nchi
imetulia na inasonga mbele, kamwe hautasahaulika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
nafasi zote za Uwaziri alizozishikilia katika kipindi hicho, kwanza
kama Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba na baadaye kama Waziri wa
Elimu, alijithibitisha na kujipambanua kama Mzalendo wa kweli kweli wa
Kenya na mpenzi halisi wa nchi yake.”
Ameongeza Rais: “Nakutumia
Mheshimiwa Rais salamu zangu za rambirambi na zile za Serikali yangu
kufuatia msiba huu. Aidha, kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu
kwa familia ya Mheshimiwa Kilonzo. Nataka wajue kuwa niko nao katika
kipindi hiki kigumu cha majonzi na naungana nao kuomboleza na kumwomba
Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Mutula Kilonzo.Amin.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM