Shibuda atishia kuandamana na ng'ombe hadi ikulu... Adai eti zinanyanyaswa
Mbunge
wa Maswa Magharibi, John Shibuda anatarajia kuongoza maandamano makubwa
ya ng’ombe kutoka Lusumo Nyakabanga Mkoani Kagera, hadi Ikulu kwa Rais
Jakaya Kikwete ili kupinga uonevu na manyanyaso wanayofanyiwa wafugaji.
“Kama watu
wanasema ni porojo za Shibuda, basi wasubiri kama hotuba ya Waziri Mkuu
haitakuwa na majibu kwa wafugaji, lazima hayo yatatokea kwa mara ya
kwanza katika historia ya nchi yetu, hawa nao ni binadamu waambiwe basi
kama hawatakiwi Tanzania,” alisisitiza.
Mbunge huyo
alitoa kauli hiyo juzi akiwa na uongozi wa wafugaji kutoka Kanda ya Ziwa
ambao wako Dodoma kwa lengo la kuonana na Mawaziri wa Maliasili na
Mawaziri wa Mifugo akiwemo Waziri Mkuu, ili kufikisha kilio cha wafugaji
ambao wanateketezewa mifugo yao na askari wa wanyama pori.
Shibuda alisema kuwa “Katika
nchi yoyote duniani hakuna mateso yanayofanywa kwa wananchi wake kama
ambavyo inafanyika Tanzania kwa upande wa wafugaji, ni heri ya wakimbizi
watakuwa na amani kuliko hawa wanaonekana kama takataka.”