Akizungumzia
suala la mashine za kura bungeni, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe, amesema utaratibu unaotumika sasa wa kura za
ndiyo na hapana ni wa zamani na hautendi haki, kwani huegemea zaidi
katika uamuzi wa Spika na si wabunge.
“Lakini Bunge letu lina vifaa vinavyoonesha namna ya
kupiga
kura na kuonekana kwenye meza ya Spika, tena yapo maelekezo
yanayomwezesha mbunge husika jina lake lionekane au la, sasa sielewi kwa
nini bado tunang’ang’ania mfumo wa ndiyo na hapana, hapa kuna mchezo
mchafu,” alisisitiza.
Alisema
mfumo huo ukitumika, utaongeza uhuru wa wabunge kupiga kura bila kujali
itikadi za vyama na kutanguliza maendeleo ya wananchi, kwani kwa sasa
mtindo wa kura za “ndiyo“ na “hapana” hufanya Wabunge wengine washindwe
kutoa uamuzi sahihi kwa hofu ya kuitwa wasaliti.
Pamoja
na hayo, Mbowe alisema kambi ya upinzani inaitaka Serikali iwasilishe
utekelezaji wa maazimio kuhusu suala la Richmond, ripoti ya Jairo,
maazimio ya kamati ndogo ya Maliasili na Utalii kuhusu usafirishaji wa
twiga na wanyama wengine hai na suala la mabilioni ya fedha yaliyofichwa
Uswisi.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumzana waandishi wa habari mjini Dodoma hapo jana.