Chama Cha
Wananchi (CUF), kimesema vurugu zinazoendelea bungeni zinasababishwa na
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kushindwa kujenga hoja
na mbinu za kuwabana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alisema wabunge wa Chadema wana tabia ya kufuata mfumo
wa kwenda bungeni na hoja zinazobeba chama chao na si za Watanzania wote
kama jinsi CCM wanavyofanya.
“Kambi rasmi ya upinzani imepoteza uwezo wa kujenga hoja za mashiko na
mbinu madhubuti za kuwabana wabunge wa CCM bungeni na badala yake
Chadema, wamekuwa na tabia mbaya ya kubeba chama chao,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema kambi rasmi ya upinzani pia imeshindwa kulinda utaratibu mzuri
wa kutetea masilahi ya umma bila jazba na hoja zenye mashiko kama
ilivyokuwa miaka ya nyuma ilipokuwa ikiongozwa na CUF, Kiongozi huyo
alisema kambi ya upinzani inapaswa ijipange upya kwa utaratibu na
mikakati mizuri ya kuteta hoja za wananchi bila kuyumbishwa na wabunge
wa CCM.
“Bunge usiwe uwanja wa kuonyesha mbwembwe za chama bali uwe uwanja wa
kutetea haki za wananchi, wabunge wanapaswa wabadilishe mitazamo ya
kuona bungeni ni sehemu ya kujionyesha kisiasa na chama chako kinafanya
nini nje ya Bunge,” alisema Lipumba.
Alisema viongozi wa Serikali wanapaswa kubadilika kuhusu namna ya kutoa majibu bungeni.
Profesa Lipumba alisema mawaziri wengi wanakuwa wakitoa majibu mepesi
katika maswali ya msingi yanayoulizwa na wabunge wa upinzani.
Alisema Bunge linatumia muda na pesa za walipakodi vibaya kwa baadhi ya
wabunge kuwa na ubishi usiokuwa na tija, kutoleana matusi na wengine
kuingilia hoja za wenzao bila sababu za msingi.
Profesa Lipumba pia alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda amepoteza uwezo wa kuliongoza Bunge.