Waziri
wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk
akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za usafiri
ya China (CITS) Zou Wang Sheng (mwenye fulana nyekudu) kushoto ya Sheng
ni Balozi mdogo wa China Madam Chen huko Ofisini kwake Kikwajuni Mjini
Zanzibar.
Waziri
wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk
akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za
usafiri ya China (CITS) Zou Wang Sheng baada ya mazungumzo yao huko
Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo
Zanzibar
………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Kuokosekana
kwa Matangazo ya Vivutio vya Zanzibar nchini China kumetajwa kuwa
sababu inayopelekea Watalii wanaotoka nchini huko kushindwa kuja
Zanzibar kufanya shughuli za Utalii.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za usafiri ya China (CITS) Zou Wang
Sheng ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Habari
Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk huko Ofisini kwake
Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Sheng
amesema China ni miongoni mwa nchi zinazotoa Wataii wengi kutembelea
nchi tofauti duniani lakini Wachina walio wengi hushindwa kuja Zanzibar
kutokana na kukosa taarifa zinazohusu vivutio hivyo.
Amedai
kuwa hata katika Balozi ya Tanzania nchini China hakuna Matangazo
yanayohusu vivutio vya Zanzibar badala yake kunapatikana Matangazo ya
Mbuga za Serengeti na Manyara ambazo zote ziko Tanzania Bara.
Sheng
ambaye ni mara yake ya kwanza kuja Zanzibar ameongeza kuwa kutokana na
mazigira mazuri yakitalii yaliyopo Zanzibar anaamini kama kutafanywa
mkakati thabiti wa kuvitangaza Vivutio vya Zanzibar hapana shaka zaidi
ya Watalii 200,000 wanaweza kuitembelea Zanzibar kwa mwaka.
Ameelezea
kuvutiwa kwao na Fukwe, hali ya hewa na mazingira ya Zanzibar kwa
ujumla wake na kuahidi atakaporudi atafanya kazi ya kushawishi makundi
ya Wageni kuja kujionea vivutio hivyo.
“Tumetembea
nchi nyingi dunia kufanya ziara za kitalii lakini ukweli nikwamba ni
nchi chache sana za visiwa duniani zenye vivutio vizuri kama Zanzibar ”
Alisema Sheng
Awali
Waziri wa habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema
Zanzibar na China zimekuwa na mashirikiano makubwa kwa muda mrefu hasa
katika sekta za elimu, Afya na teknolojia na kwamba kwa sasa Sekta ya
Utalii inapaswa kupewa mkazo wa pekee.
Ameongeza
kuwa Zanzibar imekuwa ikipokea Watalii kutoka nchi nyingi za Ulaya na
hasa Wataliano na kwamba umefika muda sasa walau Theluthi ya Watalii
kutoka China kuja kutembelea Zanzibar.
“Taarifa
zinaonesha China inatoa Watalii zaidi ya Milioni moja kwenda kutembelea
nchi tofauti duniani sasa tunataka walau watalii laki tatu watembelee
Zanzibar kwa mwaka ” Ameongeza Waziri Mbarouk.
Ameongeza
kuwa mazingira ya Zanzibar ni mazuri kwa vivutio vingi vya utalii na
hali ya kisiasa ilivyotengamaa na kulitaka Shirika hilo kufanya jitihada
zake ili kuwepo kwa Safari za ndege zinazotoka China na kuja Zanzibar.
Waziri
Mbarouk amewahakikishia Wawekezaji hao kila aina ya ushirikiano ili
kuona Sekta ya Utalii nchini inasonga mbele kupitia Watalii wa kichina.
Kwa
upande wake Balozi mdogo wa China nchini Madam Chen Queman amesema kuwa
walipokea ushauri kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Menyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kusaidia kuitangaza Zanzibar ambapo
ujio wa kampuni hiyo ni utekelezaji wa shauri hilo.
Ameongeza
kuwa njia pekee ya kufikia malengo yaliyokusudiwa ni kuhakikisha
kunakuwepo mawasiliano na mashirikiano ya moja kwa moja kati ya Kampuni
hiyo na Mamlaka ya Ukuzaji Vitegauchumi Zanzibar ZIPA.
Madam
Chen amesema ZIPA ndio watakao kuwa Wenyeji wa Kampuni hiyo ili kujua
nini kifanyike katika hatua za mwanzo kuhakikisha Zanzibar inafaidika na
Watalii kutoka nchi ya China.