Potiskum,
Nigeria (AP) – Waislamu wenye siasa kali wamewaua wanafunzi 29 na
mwalimu mmoja katika shambulio kwenye shule ya bweni Kaskazini-mashariki
ya Nigeria.
Baadhi ya
waathirika ambao bado wanatibiwa majeraha ya risasi na kuchomwa moto
wamesema baadhi ya wanafunzi walichomwa moto wakiwa hai katika shambulio
hilo kabla ya alfajiri ya Jumamosi (leo) katika shule ya sekondari ya
serikali iliyopo mjini Mamudo jimboni Yobe.
Huku
akitokwa na machozi ya uchungu pembeni ya miili ya wavulana wake wawili,
mkulima Malam Abdullahi aliapa kuwaondoa wanae watatu waliobaki katika
shule ya jirani.
Alilalamika kwamba kulikuwa hakuna ulinzi kwa ajili ya wanafunzi
licha ya kupelekwa kwa maelfu ya askari tangu serikali ilipotangaza hali
ya dharura katikati ya Mei katika majimbo matatu ya
Kaskazini-mashariki.
Shule
nyingi zimechomwa moto na idadi kubwa ya wanafunzi kuuawa wakiwamo zaidi
ya waathirika 1,600 waliouawa na Waislamu hao wenye siasa kali tangu
2010.