Balozi
na mwakilishi wa kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa ameitaka jamii
ya kimataifa iyalazimishe makundi ya waasi ya Darfur kukaa katika meza
moja ya mazungumzo na serikali ya Khartoum. Daffa Allah Alial-Haj
ameitaka jamii ya kimataifa iisaidie nchi yake katika mchakato wa
kurejesha amani na utulivu katika jimbo la Darfur.
Amesema,
ili kufikia lengo hilo, jamii ya kimataifa inapaswa kuyalazimisha
makundi ya waasi yasitishe vitendo vya utumiaji mabavu na kukaa katika
meza moja ya mazungumzo na serikali ya Sudan. Balozi na mwakilishi wa
kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa amesema, serikali ya Khartoum
inaendelea na juhudi zake za kuyakalisha katika meza moja ya mazungumzo
makundi ya waasi lakini jamii ya kimataifa inapaswa kuisaidia nchi yake
katika hilo. Jimbo la Dafur lililoko magharibi mwa Sudan limekuwa
likikabiliwa na hali ya mchafukoge tangu mwaka 2003.