Rais
wa Ujerumani Joachim Gauck ametoa ujumbe wa kumuunga mkono Edward
Snowden, mfanyakazi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA
aliyefichua siri za ujasusi unaofanywa na shirika hilo kuwa ni mtu
anayestahili heshima kwa kutetea uhuru wa faragha wa mtu binafsi. Gauck
ametoa kauli hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti moja la
Ujerumani. “Mtu yeyote anayetoa taarifa kwa umma na kuchukua hatua
kutokana na dhamiri ya nafsi yake anastahili heshima”, amesema Rais huyo
wa Ujerumani. Ameongeza kuwa tangu mwezi uliopita wa Juni wakati
Snowden alipofichua taarifa za shughuli za ujasusi
unaofanywa
na Marekani, binafsi amekuwa na mashaka makubwa na wasiwasi wa kuchelea
kama kuna usalama kwa yeye kutuma barua pepe na kuzungumza kwa uwazi
kabisa kwa kutumia njia ya simu. Rais wa Ujerumani ameongeza kama
ninavyomnukuu: “hofu ya kuchelea kunaswa na kuhifadhiwa na mashirika ya
kigeni ya ujasusi mazungumzo yetu ya simu au barua pepe yanabana hisia
zetu za kujihisi kuwa tuko huru na wenye faragha”. Rais wa Ujerumani
ameitaka serikali ya Kansela wa nchi hiyo Angela Merkel ifikie
makubaliano na waitifaki wake yatakayoheshimiwa ya kudhamini uhuru wa
faragha wa watu. Edward Snowden alifichua kuwa mashirika ya ujasusi ya
Marekani hufanya udukuzi kote duniani kwa kutumia mbinu ya kiteknolojia
ya siri kuchunguza mawasiliano ya simu ya watu, barua pepe na
mawasiliano mengine.