Uongozi
wa jiji la Dar es salaam umesisitiza nia yake ya kusafisha jiji hilo
licha ya watu wengi kuamini kuwa zoezi hilo lilitiliwa mkazo zaidi
wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Marekani, Barrack Obama.
Hayo
yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mheshimiwa, SAID MECK
SADIC, wakati akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari nchini mapema
leo asubuhi, ambapo ameweka wazi mipango ya serikali kuendeleza usafi
katika jiji, huku akisisitiza kuwa tayari ameshakutana na viongozi wake
kupanga mikakati hiyo.
“Sisi
tumejipanga sawasawa, usafi sio mpaka waje wageni, hapana kwa kweli!
nimeshakaa na Meya wajiji na viongozi wengine na kukubaliana kuongeza
juhudi zaidi za kulisafisha jiji letu”. Alisema Mheshimiwa Sadick.
SADICK
aliongeza kuwa ujio wa Mheshimiwa Obama sio sababu pekee iliyosababisha
serikali ya mkoa huo kusafisha jiji, bali walikuwa na mipango hiyo
kabla ya ujio wa ugeni huo mzito kwa Taifa, na bahati nzuri zoezi
likaboreshwa zaidi baada ya ziara ya Rais wa Marekani kuwepo.
Aidha
SADICK aliwataka watu wanaopotosha Umma kuwa nguvu ya serikali ya
kusafisha jiji ni nguvu ya soda, bali amewaomba wananchi kutoa
ushirikiano mkubwa ili kuliweka jiji katika hali ya usafi tofauti na
siku za nyuma.
SADICK
alisisitiza kuwa kama kuna mtu ana amini kuwa zoezi hilo ni nguvu ya
soda, basi ajaribu kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na uongozi, na
baada ya hapo hiyo nguvu ya soda itaonekana.
Hata
hivyo, SADICK alisema suala la usafi ni muhimu kwa afya ya binadamu,
hivyo ni wajibu wa kila mkazi wa jiji kutambua hilo na kukubali kutunza
mazingira ili aepukane na magonjwa mbalimbali.
Siku
za karibuni, jiji la Dar es salaam ambalo linapondwa na watu wengi kuwa
chafu limebadilika ghafla na kuwa safi kufuatia serikali kulisafisha
kwa juhudi zaidi wakati wa ujio wa Rais wa Marekani Barrack Obama.