Askari wa Tanzania wa Kikosi cha Kulinda Amani Darfur wakiwa
wamelazwa mjini Khor Abeche, Sudan juzi baada ya kunusurika kuuawa
katika shambulizi lililofanywa na waasi na kusababisha wenzao saba
kuuawa na wengine 14 kujeruhiwa. Picha na UNAMID.
Dar
es Salaam. Wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likiwa bado
halijatangaza rasmi majina ya wapiganaji wake waliofariki huko Sudan,
askari polisi aliyeko huko ameeleza chanzo na mazingira ya tukio hilo.
Wapiganaji saba na wengine 14 walijeruhiwa Jumamosi iliyopita.
Gazeti
hili limepata majina ya askari hao waliofariki kutoka vyanzo tofauti
lakini limeshindwa kuwataja leo kwa kuwa JWTZ kupitia kwa msemaji wake,
Kanali Kapambala Mgawe limesisitiza kuwa haliwezi kutangaza majina hayo
hadi litakapowasiliana na jamaa za askari waliofariki.
Tukio lilivyotokea
Akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina, askari polisi huyo anayefanya kazi katika
Mji wa Nyala uliopo Darfur, alisema mauaji hayo yalitokea wakati askari
hao walipokuwa wakifuatilia magari yao yaliyokuwa yameporwa na kundi
mojawapo la waasi.
Usalama
katika Mji wa Nyala ambao ndiyo mkubwa zaidi katika eneo la Darfur,
umekuwa mdogo katika siku za hivi karibuni. “Wale wanajeshi walikuwa
doria ya kawaida, ila kama wiki moja iliyopita waasi walivamia tena
doria ya wanajeshi wetu na kupora magari manne bila kuua mtu.
“Siku
ya mauaji hayo wanajeshi wetu wakiwa tena katika doria waliyaona yale
magari yaliyoporwa kwa mbali yamepaki, waliyafuatilia, walipokaribia
kumbe ulikuwa mtego, wakashambuliwa,” alisema askari huyo na kuongeza:
“Mauaji hayo yametokea takriban kilometa 70 kutoka katika kambi niliyopo
mimi, lakini wote tupo eneo la kusini na hiyo kambi ya Korabeche
inaongozwa na jeshi letu.”
Tofauti
na chanzo chetu cha habari huko Darfur, Kanali Mgawe alisema wanajeshi
hao walishambuliwa walipokuwa kwenye msafara wa kusindikiza walinzi wa
amani.
Makundi yanayopambana
Askari
huyo aliyeko Darfur alisema: “Makundi yanayopambana huku yapo mengi ila
makubwa yapo kama matano. Kuna moja linaitwa Jeshi la Ukombozi la Watu
wa Sudan (SPLA), ambalo limegawanyika katika makundi mawili pia kuna
mengine kama JEM, Janjaweed na mengineyo.”
Akizungumzia
mshtuko walioupata baada ya mauaji hayo, askari huyo alisema
wafanyakazi wote wanaohusika na ulinzi wa amani wamepatwa na ganzi...
“Huku kwa kweli hali imekuwa chungu, tangu askari hao wauawe hali
haitabiriki kabisa, tupo nje hapa (hospitali walimohifadhiwa),
tunasubiri uhakika.”
“Hawa
jamaa (waasi), wamesheheni silaha na wana vifaa vya kisasa kiasi kwamba
hata ndugu zetu walizidiwa kutokana na wenzao kuwa na silaha nzito,
nikija Tanzania nitakuonyesha picha za mapambano yao,” alisema.
Akizungumzia
kazi ambazo polisi wanazifanya huko, alisema hawaruhusiwi kushika
silaha, bali kuwashirikisha wananchi katika masuala ya amani.
“Sisi
majukumu yetu ni kuungana na jamii na kuwafundisha masuala mbalimbali,
hivyo sisi tunawasiliana moja kwa moja na wananchi waliopoteza makazi
kisha tunaandaa taarifa. Haturuhusiwi kushika silaha, wanajeshi wao
wanatulinda na kusimamia usalama na kutusindikiza wakati wa doria,”
alisema.
“Huku hali ya usalama haitabiriki. Mpaka sokoni tunakwenda chini ya ulinzi.”
Kauli ya JWTZ
Akizungumza
kwa simu jana, Kanali Mgawe alikanusha uvumi wa majina yaliyosambaa
mitandaoni huku akisema kwa utaratibu uliopo, jeshi haliwezi kutangaza
majina hayo hadi ndugu watakapotaarifiwa. “Hayo majina yanayotajwa
kwenye mitandao ni ya uongo. Kwa sasa mimi sijaletewa majina na
utaratibu uliopo ni hadi ‘next of kin’ (ndugu) wao wajulishwe kwanza,”
alidai Kanali Mgawe.
Hata
hivyo, alisema Tanzania imewasilisha maombi ya kubadilisha kanuni za
kulinda amani ikitaka kuruhusiwa kujihami kwa silaha za moto pale
wanajeshi wake wanaposhambuliwa kwa kutumia kanuni namba saba ya Sheria
za Majeshi ya Kulinda Amani.
Mwananchi