Friday, July 12, 2013
Neymar hatarini kuburuzwa Kortini.
Kampuni ya masuala ya masoko ya michezo DIS ambayo pia inamiliki supermarket nchini Brazil imetishia kumburuza nyota wa Brazil aliyesajiliwa na klabu ya Barcelona hivi karibuni Neymar kwa kile ilichokiita kudhulumiwa haki yake katika mauzo ya mchezaji huyo .
DIS inadai kuwa ilikuwa inamiliki haki za Neymar kwa asilimia 40% na ilikuwa na haki ya kupata fedha kwenye mauzo ya mchezaji huyo lakini hadi sasa hakujawa na mawasiliano yoyote baina ya kampuni hiyo na wawakilishi wa Neymar hali inayowafanya kuwa na wasiwasi wa kupata haki yao.
Kwa mujibu wa mahojiano maalum yaliyofanywa baina ya kiongozi wa kampuni hiyo na kituo cha habari cha Marekani cha Bloomberg , DIS inapaswa kulipwa fedha kutokana na Euro milioni 57 ilizolipwa Santos baada ya kumuuza Neymar , pamoja na Euro Milioni mbili kama Neymar akichaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji watatu wanaowania tuzo ya Mchezaji bora wa dunia ya Ballon D’or pamoja na fedha nyingine zaidi zitakazotokana na mazuo ya tiketi kwenye mechi mbili za kirafiki baina ya Santos na Barcelona ambazo ni sehemu ya makubaliano ya mauzo ya mchezaji huyo ambapo kama mechi hizo hazitachezwa Barcelona italazimika kulipa fidia ya Euro milioni 4.
Kampuni hiyo imesema kuwa itafanya mazungumzo na Santos kabla ya kuchukua hatua za kisheria ambapo itawashitaki Barcelona pamoja na Neymar mwenyewe kwa kukiuka makubaliano ya kimkataba .
Barcelona ilimununua Neymar kwa Euro Milioni 57 ambapo ripoti kadhaa zimedai kuwa Santos imeambulia Euro Milioni 9 pekee kwenye mauzo hayo huku fedha nyingine zikienda kwa makampuni kadhaa na watu binafsi ambao walikuwa wanamiliki sehemu au asilimia za haki za mchezaji huyo .
Utata huu kwenye mauzo ya Neymar unatokana na Umiliki wa mtu wa tatu ambao umezoeleka kwenye bara la Amerika ya kusini ambako mara kadhaa watu binafsi na makampuni humiliki sehemu ya haki za wachezaji hali ambayo mara nyingi huleta utata pale mchezaji husika anapouzwa .