Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya City mjini Dodoma, Shaban Pili (18), akiwa katika wodi namba moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. |
Mwanafunzi
wa Chuo cha Ufundi (Veta) mkoani Dodoma, Taliki Juma, (22) amefariki
dunia baada ya kujilipua kwa kutumia mafuta ya petroli na kujeruhi
wengine nane.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 10.30 jioni Nzuguni eneo la Machaka, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma Mjini.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda, jana alisema
Taliki alijilipua katika saluni inayomilikiwa na Irene Mapunda
inayojulikana kwa jina la Tonny Hair Dressing Saloon.
Alisema mwanafunzi huyo aliyekuwa akisomea fani ya ufundi magari,
alienda kununua Petroli lita tano katika kituo cha Mafuta cha Nanenane
na kuimwaga ndani ya chumba cha Saluni ya Irene.
“Watu waliokuwa karibu naye walijaribu kumsihi asijilipue lakini
hawakufanikiwa kwani Taliki aliwasha kibiriti ndani ya saluni hiyo na
kusababisha moto mkubwa kulipuka ambao uliwaunguza wote waliokuwa karibu
naye pamoja na mali zote zilizokuwa ndani ya Saluni hiyo,” alisema.
Aliwataja
majeruhi hao kuwa ni Mugina Hussein (32), Swaibu Kassimu (20), Easte
Silau (30) na Fredrick Gabriel (21), wote wafanyabiashara na wakazi wa
Nzuguni.
Wengine ni mwanafunzi wa darasa la nne Benson Mushi (11), Japhet Japhet
(18), Meshack John (18) na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari ya City, Shaban Pili (18).
Alisema majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
ambapo nane wamelazwa wodi namba moja ya wanaume na mmoja amelazwa wodi
namba 10 ya wanawake.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Kaganda alisema tathimini ya hasara iliyosababishwa na moto huo bado haijafahamika.
Aidha, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.
Hata hivyo, alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hili.
MUUGUZI WA ZAMU
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Magreth
Maki, alisema kuwa Taliki alifariki jana katika hospitali hiyo kutokana
na majeraha makubwa aliyopata wakati wa tukio hilo.
Hata hivyo, alisema hali ya majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo
wanaendelea vizuri isipokuwa mmoja ambaye bado hali yake si nzuri.
“Bado wanaendelea kutibiwa vidonda walivyovipata kutokana na tukio hilo,
hali yao inaendelea vizuri isipokuwa mmoja ambaye hali yake ni serious
(mbaya), “alisema Muuguzi huyo wa zamu.
MAJERUHI WANENA
Akizungumza na NIPASHE, baba mzazi wa Benson Mushi, Dickson Mushi,
alisema kuwa mwanae alikumbana na mkasa huo alipokwenda kupeleka nguo
zake kwa ajili ya kunyoosha.
“Mwanangu alikwenda karibu na saluni hiyo kwa ajili ya kwenda kunyoosha
nguo zake ndipo alipokutana na mkasa huu. Amekuwa na kawaida ya kwenda
kuonyoosha karibu na saluni hiyo,”alisema Mushi alipokuwa akizungumza na
gazeti hili nje ya wodi.
Kwa upande wake, majeruhi mwingine Shaban Pili, alisema alikumbwa na
mkasa huo katika jitihada za kumuokoa marehemu baada ya kusikia kelele
za kuomba msaada kutoka kwa wafanyabiashara waliopo jirani na saluni
hiyo.
“Tuliangaika kuvuta mlango wa saluni na tukafanikiwa, tulipomuuliza
kulikoni amejimwagia petroli, alitujibu kuwa tumwache lakini ghafla
aliwasha kiberiti na kujilipua,”alisema na kuosha mkono aliungua sana
wakati alipokuwa akimvuta marehemu nje ya saluni hiyo.
Naye majeruhi Meshack John, alisema alikuwa amekaa karibu na saluni
hiyo, ndipo alipokuja marehemu (mtoto wa baba yake mdogo) na kumuomba
ampatie Sh. 15,000.
“Nilimuuliza ya nini? Akanijibu kuwa baba kanituma (baba yake mdogo
ambaye ni mmliki wa bucha analouza nyama katika eneo la Nzuguni),
nikakataa na kuwaomba ushauri wenzangu kama nimpatie ama la,”alisema.
Hata hivyo, baada ya mashauriano ya muda mrefu akaamua kumpatia kiasi
hicho cha fedha na akaondoka zake na kwenda kununua mafuta ya petroli
lita tano.
Alisema baadaye alirejea na lita tano za mafuta na kisha kujifungia ndani ya saluni kabla ya kujimwagia.
“Akajimwagia, mama mmoja naye amelazwa hapa hapa, akasema Taliki
anajiwasha huko moto naona mafuta yanatiririka huku nje,”alisema.
Alisema hali hiyo ilisababisha wasogeze mlango wa saluni na kabla hawajachukua hatua moto ukaanza kuwaka.
“Tulikuwa majeruhi tisa lakini mwenzetu Taliki alifariki dunia leo
asubuhi kwa kuwa yeye alijimwagia mafuta kabla kujilipua moto,”alisema.
Kwa upande wa chanzo la tukio hilo, alisema kuwa marehemu alikuwa na
ugomvi na wenzake ambao aliwashutumu kwamba wanamtangazia kuwa
anauhusiano wa kimapenzi na mmiliki wa saluni hiyo (Irene).
“Walikuwa wanamtangazia kuwa amekuwa akimhonga (mmiliki wa saluni)
pesa…Ijumaa walipigana sana na wenzake hadi alirudi nyumbani kuchukua
panga akitaka kuja kuwakatakata wenzake akidai kwanini wampakazie jambo
ambalo halina ukweli,”alisema.
Majeruhi huyo alisema ilimbidi kwenda kuamulia ugomvi huo na ukaisha
lakini alishangaa tena juzi marehemu aliamua kuchukua uamuzi huo.
Naye Silau, aliyelazwa wodi namba 10, alisema alikuwa akifanya biashara
karibu na saluni hiyo ndipo moto ulipomrukia na kumuunguza mikononi.
“Mimi nilisikia harufu ya mafuta ya petroli na kuwaambia wenzangu kuwa
nasikia harufu katika saluni hiyo lakini sikusogea karibu,”alisema
Silau.
MASHUHUDA
Mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini
walisema kuwa marehemu huyo alipelekwa hospitali akiwa ameungua vibaya
kiasi cha ngozi yote kuchunika.
“Marehemu alikuwa akilalamika maumivu, akisema anatamani kufa mapema
maana maumivu ni makali sana,”alisema mmoja wa shuhuda wa tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE