Rais
Jakaya Kikwete jana alipuliza kipenga kuzindua Tamasha la Matumaini Dar
es Salaam na kuwanyooshea kidole viongozi wa dini wanaohubiri siasa
katika maeneo ya ibada akisema kufanya hivyo ni kufilisika kifikra.
Akizungumza
muda mfupi kabla ya kupiga filimbi kuashiria ufunguzi wa tamasha hilo
lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Rais Kikwete
alisema ni jambo la hatari kwa Watanzania kukubali kugawanywa kwa
misingi ya udini, rangi au maeneo wanakotoka.
Alitaka
dini zitumike kuwaunganisha wananchi na siyo kuwagawanya akisema
Watanzania wanakwenda makanisani na misikitini kusali na siyo kufanya
siasa. Alisema kiongozi yeyote wa dini anayesisitiza waumini wake kuunga
mkono chama chochote cha siasa amefilisika kifikra.
“Ni
hatari tukigawanyika, ni lazima tuwaambie watu wanaotaka kutugawanya
kwa misingi ya dini, rangi au maeneo tunakotoka kwamba hatutaki na wala
hatukubali. Nchi hii wakoloni waliishindwa hivyo lazima tuendeleze
utamaduni wa kukataa kugawanywa kwa msingi wowote ule,” alisema Rais
Kikwete.
Aliwataka
wanasiasa kuepuka kauli zenye kuchochea vurugu miongoni mwa wananchi
wanapokuwa kwenye harakati zao za kisiasa akisema madaraka ya kisiasa
yatafutwe kwa njia ya amani na siyo kuingiza kauli za uchochezi zenye
kuwagawa wananchi.
“Nawaasa
wanasiasa wasipandikize chuki za kidini au maeneo wanakotoka wananchi,
kama ni madaraka yatafutwe kwa njia ya amani kwenye sanduku la kura,”
alisema Rais. Alisema Tamasha la Matumaini liwe mfano wa kuigwa wa
kutumia michezo kuwaunganisha watu badala ya kuwagawanya.
Alisema
timu zilizotumbuiza jana zilimebeba majina ya Simba na Yanga,
zimejumuisha wabunge kutoka vyama vyote ikionyesha kuwa wote ni wamoja
licha ya tofauti za kisiasa.
Alipongeza
mkakati wa waandaaji wa tamasha hilo ambao wametangaza kwamba mapato
yatakayopatikana yatatumika kusaidia shule za sekondari katika mikoa
minane nchini.