Mbeya. Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Sekondari ya Ilomba Jijini Mbeya,
Emanuel Komba(15) amenusurika kuuawa na watu wasiojulikana baada ya
kutekwa, kufungwa kamba mikononi na kuzibwa vitambaa mdomoni na kisha
kutupwa kwenye korongo lililopo eneo la Mlimanyoka .
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakaeli Masaki alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari kijana huyo anachukuliwa maelezo kwenye kituo cha polisi wilayani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 10:30 na kwamba aliokotwa na wasamaria wema na kumkimbiza kwenye kitengo cha huduma ya haraka kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kwamba hali yake inaendelea vizuri. Akizungumza na gazeti hili, Komba alisema siku ya tukio alikuwa anatoka shuleni na kwamba alikuwa akitumia usafiri wa baiskeli ambayo ghafla iliharibika na kwamba alipokuwa katika harakati za kuitengeneza ghafla lilitokea gari aina ya roli likiwa na rangi ya njano na mtu mmoja kumwamuru kupanda katika gari hilo kwa kumuahidi kumsaidia kutengeneza.
“Nilipopanda ndani nilishangaa kuwaona wanaume watatu wakiwa wamemshikilia kijana ambaye kwa haraka alikuwa sawa na mimi wakimchoma kitu kama sindano na pembeni yake kulikuwa na kopo lenye damu,” alisema Emanuel.
Alisema, wakati wanaume hao wakiendelea na zoezi hilo, alifanikiwa kuangalia kwa dereva na kuona wapo wawili na alipokuwa akiendelea kushangaa alisikia sauti ikimtaka asipige kelele na kama hatatekeleza agizo hilo watamfanya kama wanavyomfanya mwenzake.
“Nilishangaa ghafla nilipigwa kibao na kushindwa kufahamu kilichoendelea, mpaka leo nilipojikuta nikizungukwa na watu wa eneo hili la Mlimanyoka,”alisema
Alisema, alifanikiwa kutoa namba za mama yake, huku akiwaeleza kuwa kwenye gari alililokuwa amepanda kulikuwa na mwenzake aliyekuwa akitolewa damu na watu hao.
Credit:Mwananchi