FAMILIA ya Nelson Mandela, ambaye yu mahututi katika hospitali ya
Medi-Clinic jijini Pretoria kwa zaidi ya mwezi sasa, inaweza katika siku
au wiki kadhaa zijazo ikakabiliwa na uamuzi mgumu ambao umeshapata
kuzikuta familia zingine katika matumizi ya mashine kuwezesha uhai:
unapofika wakati wa kusema inatosha.
Wataalamu wa tiba ndani na nje ya nchi ambao hawajihusishi na chochote
katika huduma ya kiongozi huyo mstaafu, zimeichukulia taarifa ya
Serikali – kwamba Mandela ana hali mbaya lakini yu imara-kumaanisha
kwamba anasaidiwa tu na vifaa ambavyo, kutokana na umri wake mkubwa,
vitawafanya ndugu, madaktari na nchi kuwa na uamuzi mgumu wa juu ya
kuendelea kumweka hai kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 94.
Uamuzi wowote utaangaliwa kwa udadisi mkubwa na dunia na kuhusisha ndugu
wengine ambao wameonekana kuingia katika msuguano juu ya uamuzi kuhusu
urithi, eneo atakakozikwa na mali zake atakazoacha.
Na itafanyika hivyo chini ya sheria za Afrika Kusini na uamuzi wa
mahakama ambao unaacha maswali katika maeneo mengine ya nani atachukua
uamuzi. Katika hali ambayo mgonjwa ameacha wosia au ameteua mtu wa
kuamua kwa niaba yake, uamuzi uko wazi.
Lakini kama hakuna wosia au mtu wa kuamua kwa niaba yake au kuna zaidi
ya mtu mmoja wa kuamua-kama watoto au wanafamilia wengine kama alionao
Mandela – sheria ya Afrika Kusini haiko wazi, wataalamu wa sheria nchini
wanasema. “Si jambo rahisi hasa unapokuwa unakabiliwa na ugomvi ndani
ya familia ambao unakuwa umeshaenea mpaka nje,” anasema Nomboniso Gasa,
mchambuzi wa masula ya siasa na utamaduni jijini hapa.
“Bado, licha ya msuguano huo na mapambano, familia ya Mandela inaonekana
bado iko imara, nadhani wanajua fika kwamba uamuzi wa kukomesha uhai
unatakiwa kuchukuliwa. Lakini hadhi ya mkusudiwa inafanya uamuzi kuwa
mgumu.”
Huu pia ni wakati ambao vifaa vya kupumulia, mirija ya kulia na mashine
zingine za teknolojia ya hali ya juu, vinaweza kuweka watu hai-hata
walio katika hali ya kutojitambua-kwa miezi hata miaka, kama ilivyo kwa
Ariel Sharon, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel mwenye umri wa miaka 84
ambaye amekuwa katika hali ya kutojitambua tangu apate kiharusi mwaka
2006.
Haijulikani vya kutosha, juu ya afya ya Mandela hasa kujua kwa uhakika
kwamba hali yake hiyo itaangukia chini ya sheria ya Afrika Kusini,
wataalamu wa sheria ya masuala ya tiba wanasema.
Kiapo cha mahakama kilichowasilishwa Juni katika mgogoro wa familia juu
ya wapi Mandela atazikwa, kilidai kuwa alikuwa katika hali ya
kutojitambua, lakini familia na timu ya madaktari walikanusha hilo.
Hakika, wanafamilia na marafiki ambao wameshamtembelea katika siku za
karibuni, wanasema Mandela wakati mwingine huzinduka, akatabasamu,
akawasiliana kwa macho, hata akajaribu kuzungumza.
Rais Jacob Zuma, ambaye alimtembelea Jumatano, alisema hivi sasa mwili
wake unakubali matibabu. Lakini hata hivyo, hakuna ubishi kwamba hali ya
kiongozi huyo ni mbaya na bado kuna shaka na kile ambacho Serikali na
familia yake wanasema juu ya hali yake.
“Naamini, binafsi, kuna kutoaminiana katika suala hili,” alisema Cheryl
Webb, mshauri wa Kituo cha Ushauri cha Masuala ya Kifamilia cha Cape
Town ambaye alishahudumia familia yenye mazingira kama hayo.
“Unapata hisia, kwamba ukweli hausemwi. Tuna uchaguzi mkuu unakuja hivi
karibuni. Kuna kauli kuwa huenda kukatokea machafuko nchini baada ya
Mandela kufariki dunia.
Kuna viashiria vingi.” Hisia kama hizo ni za kawaida. “Si muda mrefu
sana, nilipata kuambiwa kwa uhakika na watu maarufu, kwamba Mandela
amefariki dunia,” alisema Bonita Meyersfeld, Mkurugenzi wa Kituo cha
Masomo ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand jijini hapa.
“Kuna upotoshaji mkubwa wa taarifa. Nelson Mandela ni mtu mashuhuri,
lakini hivi sasa ni mashuhuri kwa ajili ya upotoshaji na kuficha mambo.”
Gazeti la The Mail & Guardian la nchini lilisharipoti, kwamba
Mandela hana wosia ulioandikwa. Familia yake haijakanusha hilo, ingawa
wanafamilia kwa kiasi kikubwa wamekataa kutoa maelezo ya kina juu ya
masuala yanayozunguka ugonjwa wake.
Na pia haijulikani kama Mandela ameteua mtu wa kufanya uamuzi kwa niaba
yake akiwa hai au marehemu – kama vile mkewe, Graca Machel-kama hatakuwa
na uwezo wa kuutoa.
Tukio kubwa lililopata kutokea katika sheria ya Afrika Kusini kuhusu
masuala ya kukatisha uhai, lilimhusu daktari Frederick Cyril Clarke,
ambaye alikwenda hospitalini jimboni Natal mwaka 1988 na kuomba
akatishwe uhai, ili aondokane na maumivu makali aliyokuwea akiyapata.
Alipata kukumbwa na mshituko wa moyo na wakati akipewa tiba hiyo ya
kukatisha uhai, ili kuokoa maisha yake kumbe, ubongo ulishakufa. Hata
hivyo aliwekwa hai kwa miaka minne. Lakini Machi 1992, mkewe aliomba
mahakama iruhusu matibabu endelevu ya mumewe huyo yasitishwe. Mahakama
ilikubali, licha ya pingamizi la Serikali.
Dk Clerk “alishapoteza uwezo wa kuishi kimwili na kiakili katika kiwango
ambacho kisingemfanya aishi kama binadamu,” mahakama iliamua.
Hivyo alirudishwa nyumbani, ambako alifariki dunia rasmi Agosti 14,
1992. Ulikuwa ni uamuzi wa kwanza na muhimu wa mahakama juu ya masuala
ya kukatisha uhai wa binadamu nchini.
Na alikuwa Mandela mwenyewe ambaye, wakati akiwa bado Rais, mwaka 1998
aliteua Tume ya Mabadiliko ya Sheria ya Afrika Kusini ili kukusanya
ripoti juu ya masuala ya kukatiza maisha. Ilibaini mianya mingi ndani ya
sheria ambayo ilipendekeza izibwe, na kwenda mbali zaidi hata
kupendekeza rasimu ya sheria ili kuziba mianya hiyo.
Sheria hiyo iliwasilishwa mbele ya Bunge mwaka 2000, lakini haikuungwa
mkono na wengi na matokeo yake, ilipuuzwa na Wizara ya Afya baada ya
Mandela kuondoka madarakani, Willem Landman, Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Maadili ya Afrika Kusini, aliandika mwaka jana katika mada
iliyoitwa “Uamuzi, Maadili na Sheria ya Kukatiza Maisha.”
Sheria ya Huduma za Afya ya mwaka 2003 ilipopita, kwa mara ya kwanza
katika sheria za Afrika Kusini ilitoa tafsiri ya kifo - kusimama kwa
shughuli zote za ubongo – hata hivyo haikugusa masuala yote ya kisheria.
Sheria hiyo haiwapi uwezo madaktari kumwondolea mgonjwa mashine
zinazomsaidia kuishi, hata bila idhini ya familia, kama mgonjwa ana
wosia wa kimaandishi na kama kazi ya ubongo imesimama, alisema Pieter
Carstens, Mkuu wa Idara ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Pretoria na
mtaalamu wa masuala ya sheria za tiba.
“Linakuwa tatizo kama mtu anatafuta maridhiano kutoka familia nzima
wakati mgonjwa hajafa ubongo, lakini hajitambui na hana wosia wa
kimaandishi au maelekezo mengine,” Carstens aliandika kupitia barua
pepe. Wakati mwingine katika masuala binafsi zaidi kama hayo nchini,
kuna mgongano kati ya kinachotakiwa na mahakama na kile ambacho mila
zinataka. Lakini kwa hili, pande hizo mbili zinakubaliana.
“Hakuna sheria mahususi ya kimila ambayo inatamka moja kwa moja kuhusu
hili,” alisema Gasa. “Kinachofanyika wakati mwingine ni kwamba ukoo
unakutana na kufanya majadiliano mafupi juu ya jinsi mpendwa wao
anavyoweza kupunguziwa maumivu.”
Kama panakuwa hapana makubaliano na timu ya madaktari inashawishika
kwamba hatua za kuokoa maisha zinatakiwa kusimamishwa, Carstens anasema,
atashauri madaktari kutafuta amri ya mahakama. Kama kuna timu yoyote ya
madaktari inaweza kuthubutu kufanya hivyo kwa mtu kama Mandela ni swali
lisilo na jibu.
“Mnataka kuhakikisha kwamba kila mmoja anaridhika, hilo ndilo lengo,”
Gasa alisema. “Lakini kwa hali hii hilo inawezekana? Hilo ndilo swali.
Hilo linaweza kufanyika sasa?”
Credit:Habari Leo