Watoto saba ambao ni raia wa Burundi na Rwanda ambao walikamatwa wakati
walipokuwa wakisafirishwa kutoka Burundi kuja Tabora kwa ajili ya kuuzwa
watumikishwe katika mashamba ya tumbaku,Watoto hawa walikamatwa eneo la
Ulyankulu wilayani Kaliua wakiwa na tajiri yao ambaye amefahamika kwa
jina la Emmanuel John(22) ambaye pia ni raia wa Burundi.
Watoto wakiwa mahakama ya hakimu mkazi Tabora wakisubiri kuingia
mahakamani kutoa ushahidi baada ya mtu aliyekuwa amewasafirisha kwa
lengo la kutaka kuwauza kukamatwa na kufikishwa Mahakamani kujibu
shitaka la kuwasafirisha kwa nia ya kuwafanyia biashara na kuingia
nchini kinyume cha sheria.
Afisa na Mwanasheria wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Tabora akiwaongoza
watoto hao kuingia chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Tabora kwa ajili
ya kutoa ushahidi dhidi ya Emmanuel John.
RAIA wa Burundi, Emmanuel John (22),aliyekamatwa akituhumiwa kusafirisha
watoto,amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa waTabora akikabiliwa na
Mashitaka mawili moja likiwa ni la kuingia nchini kinyume cha sheria na
kusafirisha binadamu kwa lengo la kutaka kuwauza.
Mbele ya Hakimu Mkazi Bw. Jackton Rushwela,Wakili wa Serikali Bw.Iddi
Mgeni, alimsomea mshitakiwa mashitaka hayo ambapo alikiri kosa la
kuingia nchini kinyume cha sheria huku kosa la pili la kuwasafirisha
watoto hao saba akijaribu kutaka kuficha ukweli.
Kutokana na kukiri kosa la kwanza, Hakimu Rushwela alimhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya sh 100,000.
Hata hivyo,mshitakiwa huyo Emmanuel John pamoja na kuiomba mahakama
impatie fursa ya kumtaarifu mkewe aliyeko huko nyumbani kwao nchini
Burundi kwa njia ya simu au apewe nafasi ya kuuza simu yake ya mkononi
aweze kulipa faini hiyo kwa nia ya kutaka kujinasua na adhabu ya kifungo
hicho cha mwaka mmoja lakini mahakama haikuwa tayari kutekeleza hilo.
Kuhusu shitaka la kusafirisha binadamu,upande wa mashitaka ulidai
mshtakiwa alikamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji akiwasafirisha
watoto Ndayisenga Batiliza(13), Ndakusenga Emmanuel(15), Nimbonajile
Nagenda(13), Yazid John(15), James Justus(14) na Samson Banteke(17).
Baadhi ya watoto hao walitoa ushahidi walidai walisafirishwa na
mshitakiwa Emmanuel John kutoka nchini Burundi na Rwanda hadi
walipokamatwa eneo la Ulyankulu wilayani Kaliua.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu itakapoendelea tena kusikilizwa kwa mashahidi wengine kutoa ushahidi wao.