Mkuu-wa-Jeshi-la-Magereza-nchini-CGP-John-Minja
---
Jeshi la Magereza
Tanzania Bara linapenda kuufahamisha Umma kwamba mnamo tarehe 23 Julai, 2013 Maafisa
wanne ambao ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza Joseph Kimaro, Sajenti Ketto
Ramadhani, Koplo Silyvester Dionice na Wada Richard Barick wa Gereza
Kiteto Mkoa wa Manyara walikamatwa na
askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati wakiwa na gari la Jeshi la
Magereza pamoja na silaha likiwa limepakia nyara za serikali. Dereva wa gari
hilo Sajenti Ketto Ramadhan alitoroka na kutelekeza gari hilo na Jeshi la
Polisi linaendelea kumtafuta.
Uchunguzi wa awali
umebaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na maadili ya Jeshi la Magereza
pamoja na sheria za uwindaji wa wanyama
pori. Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Magereza limechukua hatua zifuatazo:-
i.
Askari 3 waliohusika wamefukuzwa kazi
kwa kosa la kwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza na watafikishwa
Mahakamani baada ya upelelezi wa Polisi kukamilika.
ii.
Afisa Mrakibu Msaidizi wa Magereza
Joseph Kimaro amefunguliwa mashtaka ya kinidhamu na kusimamishwa kazi kwa kosa
la kwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza hadi maamuzi ya Mamlaka ya
kinidhamu inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) itakapotoa maamuzi dhidi
yake. Kwa sasa amezuiliwa Kituo cha Polisi Babati kusubiri kufikishwa
Mahakamani upelelezi wa Polisi utakapokamilika.
iii.
Mkuu wa Gereza Kiteto Mrakibu wa
Magereza Ally Ramadhani Sauko kwa kutumia madaraka yake vibaya amevuliwa uongozi
na kuhamishiwa Ofisi ya Mkuu wa Magereza Manyara, akisubiri maamuzi ya Mamlaka ya
kinidhamu inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) kufuatia mashtaka ya
kinidhamu yaliyofunguliwa dhidi yake.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari Ofisi ya Makao
Makuu ya Magereza
Tanzania Bara
26 Julai 2013