Taasisi ya
Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), inayodaiwa kuchangia
kuongeza ‘ walemavu’ kwa kuwakata viungo majeruhi wa ajali za boda boda,
imesema ipo tayari kuthibitisha kuwa waliokatwa viungo si madereva wa
pikipiki kama inavyodaiwa. “Anayetaka
kufahamu ukweli tuwasiliane.Takwimu za waliokatwa miguu na viungo zipo
hatuna cha kuficha tena si madereva wa pikipiki kama inavyodaiwa,”
Ofisa Uhusiano wa MOI, Almasi Jumaa, alisema.
Wanaotoa
tuhuma hizo wanadai wodi ya kuchangia huduma, waganga wanawakata miguu
majeruhi wengi wa ajali za bodaboda na hulazwa kwenye wodi maalumu
zinazojulikanazo kiutani kama ‘boda boda na Sanlg’ .
Akijibu madai hayo Jumaa aliongeza:“uamuzi wa kumkata majeruhi kiungo
haufanywi kinyemela ni makubaliano ya jopo la madaktari, hukatwa
kiungo baada ya daktari wa mgonjwa kupendekeza kwa wakuu wake ambao
huwasiliana na mabingwa wanaomchunguza mgonjwa na kuridhika kuwa ili
kuokoa maisha yake wanalazimika kuondoa kiungo.”
Alisema majeruhi wanaopokelewa MOI wanatibiwa na kuhudumiwa bila
kubaguliwa na kwamba hakuna wodi ya boda boda wala Sanlg na anayetaka
uhakika afike MOI kuthibitisha.
Aliongeza kuwa ukataji viungo huzingatia viwango vinavyokubaliwa
kimataifa na kwamba unafanyika pale ambapo mgonjwa ameumia na hawezi
kutibika.
Katika mahojiano na baadhi ya majeruhi na jamaa zao hospitalini hapo
walibainisha kuwa hawaridhishwi na moyo wa madaktari na wauguzi katika
kuhudumia wagonjwa.
Majeruhi wa boda boda walisema madaktari wanawapuuza, huchelewa kuwatibu
hali inayowasababishia maumivu makali licha ya kwamba wapo hospitalini.
Walisema kutotibiwa kwa haraka husababisha viungo kuharibika, kukatwa
na wengine kupoteza maisha na kudai kuwa katika wodi ya wagonjwa wanaochangia huduma za afya, majeruhi hulundikana kupindukia.
Walisema baadhi huambukizwa hata maradhi ya wodini pia kuna harufu
mbaya inayotokana na ama vidonda vyenye usaha sivyosafishwa au uchafu wa
shuka zilizochafuliwa na damu na pia majeruhi kutooga kutokana na
kuumia viungo.
Walidai madaktari huwakimbia wagonjwa wakitoa mfano kuwa ukifika
hospitalini hapo unapewa daktari atakayekuelekeza vipimo na dawa.
Hata hivyo baadaye tabibu huyo hutoweka na mgonjwa kupigwa dana dana
na kulazimika kumtafuta mwingine ambaye anakerwa na kuhoji sababu za
kukimbiwa na daktari wake hali inayomfanya mgonjwa kutapatapa kusaka
huduma.
Walisema jamaa za wagonjwa huzunguka kila mahali kuwatafuta madaktari ambao nao hawaonekani.
Walidai MOI haina dawa na pia hakuna gozi wala dawa za maji za kusafishia vidonda.
Baadhi walidai hakuna umakini wa kumfuatilia mgonjwa ambaye anaweza kuvalishwa mhogo (pop) mara kadhaa na mguu wake usiunge.
Pia walidai iliwahi kutokea baadhi ya wataalamu wa dawa ya usingizi
(nusu kaputi) walimwekea mgonjwa dawa kidogo na kusababisha kuzinduka
kabla ya upasuaji kukamilika.
“Walilazimika kumuongezea mgonjwa nusu kaputi iliyomzidia na kusababisha kifo ,” alidai mgonjwa mmojawapo.
UFAFANUZI
Akijibu malalamiko hayo Jumaa alisema wodi ya wagonjwa wa kuchangia
huduma ina vitanda 33 lakini idadi ya majeruhi wanaolazwa inafikia zaidi
ya 60 hali inayosababisha mlundikano na harufu wodini.
Alitoa takwimu za wagonjwa zilizoonyesha kuwa kati ya 1996-1997
waliolazwa walikuwa 5,000 wakati wagonjwa wa nje walikuwa 6,700 na kwa
mwaka 2011 na 2012 wagonjwa waliolazwa walikuwa 7,070 wakati wa nje
walikuwa 62,000.
Alisema hospitali hupokea majeruhi angalau 10 kila siku na kwamba kila
ajali kubwa majeruhi hufikishwa MOI hali inayosababisha msongamano na
foleni hata kwenye upasuaji.
Alisema hakuna uhaba wa madaktari wa mifupa na kuhudumia wagonjwa wa
ajali kama inavyodaiwa na kwamba taasisi hiyo inawasaidia majeruhi kwa
kuwapa tiba,chakula na hata kuwafikisha kwao wakipona.
habari NA GAUDENSIA MNGUMI
CHANZO: NIPASHE