- Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti hasa baada ya gazeti hili kuandika habari za mishahara kwa sekta zote, baadhi ya wafanyakazi wa taasisi za Serikali walidai kupata mishahara mipya wakati ile ya binafsi bado.
Ni ile iliyotangazwa na Serikali mwezi uliopita, ambapo inadaiwa sekta hizo nyingi zimeendelea kulipa mishahara ya zamani.
Dar es Salaam. Wafanyakazi wa
taasisi mbalimbali za Serikali wameanza kupokea mishahara mipya huku
wale wa sekta binafsi wakiendelea kupata mishahara ya zamani.
Ijumaa, Serikali ilitangaza viwango vipya vya
mishahara kwa wafanyakazi wa taasisi zake ikiwa ni wiki tatu baada ya
kutangaza viwango vya chini vya mishahara katika sekta mbalimbali
binafsi.
Kima cha chini katika taasisi za Serikali
kimepanda kutoka Sh170,000 hadi Sh240,000 huku wengine ikipanda kwa
asilimia nane wakati sekta binafsi viwango hivyo,ni vile vilivyotangazwa
na Serikali vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine kwa kuanzia
Sh40,000 hadi Sh400,000.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti hasa baada
ya gazeti hili kuandika habari za mishahara kwa sekta zote, baadhi ya
wafanyakazi wa taasisi za Serikali walidai kupata mishahara mipya
wakati ile ya binafsi bado.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema ana matumaini walimu wataanza kupokea mshahara mpya mwezi huu.
“Pamoja na kwamba mishahara bado haijalipwa lakini
tumehakikishiwa kwamba marekebisho yameshafanyika kwa ajili ya walimu
kuanza kupokea mishahara mipya mwezi huu wa Julai,” alisema Mukoba.
Aliongeza, “suala kubwa kwetu si kuanza kupokea
viwango vipya vya mishahara mwezi huu, tunachojadili sasa kiasi
kilichopandishwa, tunaendelea kufanya vikao kulijadili.”
Wafanyakazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na wao wameshapokea mishahara mipya kama
ilivyotangazwa. “Ni kweli mwezi huu nimepokea mshahara mpya,” alisema
mmoja wa wafanyakazi hao ambaye aliomba jina lisitajwe gazetini.
Mfanyakazi mwingine wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alisema
ingawa bado hawajapewa mishahara mipya lakini wamehakikishiwa kuwa
wataanza kupokea mwezi huu.
“Idara ya Uhasibu wamepewa majedwali ya viwango
vipya vya mishahara hivyo wanafanya kazi hadi usiku kuvibadilisha na
wametuhakikishia tutapewa utakapomalizika mwezi huu,” alisema.
Miongoni mwa walimu hao ambao wana shahada
walisema wana imani ya kupokea Sh600,000 badala ya Sh532,000 walizokuwa
wakizipata awali.
Kwa upande wa polisi nao ni miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali walioanza kupokea mishahara mipya kuanzia mwezi huu.
Hata hivyo wafanyakazi wa sekta hiyo waliohojiwa walisema
hawaoni dalili za kupokea mishahara mpya mwezi huu huku wengine wakikiri
kuendelea kupokea mishahara ya zamani.
“Pamoja na kwamba bado hatujalipwa mishahara,
taarifa nilizonazo ni kwamba tutaendelea kulipwa mishahara ileile ya
zamani,” alisema kwa simu mfanyakazi wa kiwanda cha Kioo Ltd.
Kauli hiyo iliungana na mfanyakazi wa Chama cha
Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) aliyesema
wamelipwa mishahara ya zamani.
“Tumeshalipwa lakini ni ile ile ya zamani, hatuoni
dalili za kupandishiwa mishahara,” alisema mfanyakazi huyo aliyeomba
asitajwe jina lake. Mfanyakazi mwingine katika Kiwanda cha Namera
alisema wameshalipwa mishahara lakini ni ile ya zamani.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi