- Jambo linalomfadhaisha na kumkasirisha zaidi ni kuona kwamba vyama hivyo tayari vimejitumbukiza tena katika madeni makubwa kutokana na viongozi wake kuendeleza ubadhirifu wa fedha na mali za vyama hivyo. Ndiyo maana Rais amelazimika kusema pasipo kupepesa macho kuwa, wengi wa viongozi wa vyama hivyo ni wezi, tena wezi wanaokula bila kunawa.
Rais Jakaya Kikwete amesema baadhi ya vyama vya
ushirika nchini vina mkusanyiko wa wezi wanaotafuna fedha za wananchi
bila hata kunawa mikono. Rais ambaye yuko mkoani Kagera kwa ziara ya
kiserikali ya siku tano, aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki mjini Bukoba
alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kufungua jengo la
kitegauchumi la Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU).
Kauli hiyo ya Rais inaonyesha dhahiri kwamba
serikali yake imekata tamaa katika juhudi zake za kuvirekebisha vyama
hivyo, baada ya muda mrefu wa ufisadi na ubadhirifu wa mali na fedha za
wanachama ambao umekuwa ukifanywa na viongozi wa vyama hivyo kwa muda
mrefu sasa.
Ni kauli iliyojaa hasira na inayoonyesha kwamba
Rais bila shaka amevunjika moyo na kukata tamaa kutokana na kukwama kwa
juhudi zake za kuvirudisha vyama hivyo vya ushirika katika mstari
nyoofu. Katika kuonyesha dhamira yake ya kuvifufua vyama hivyo, Rais
Kikwete katika muhula wake wa kwanza wa uongozi aliamua kulipa madeni
yote ya vyama vya ushirika nchini, akitarajia kwamba hatua hiyo
ingevikwamua kutoka katika madeni ambayo tayari yalikuwa yamevielemea.
Jambo linalomfadhaisha na kumkasirisha zaidi ni
kuona kwamba vyama hivyo tayari vimejitumbukiza tena katika madeni
makubwa kutokana na viongozi wake kuendeleza ubadhirifu wa fedha na mali
za vyama hivyo. Ndiyo maana Rais amelazimika kusema pasipo kupepesa
macho kuwa, wengi wa viongozi wa vyama hivyo ni wezi, tena wezi
wanaokula bila kunawa.
Tunasema hivyo tukitilia maanani kuwa, uamuzi wake
wa kulipa madeni ya vyama vya ushirika kwa kutumia fedha za walipakodi
ulikosolewa sana na wananchi ambao waliiona hatua hiyo kama mkakati wake
wa kutimiza malengo ya kisiasa, kwa maana ya kuungwa mkono na vyama
hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kitendo cha vyama hivyo
kutokomea tena katika madeni lazima kichukuliwe na Rais Kikwete kama
usaliti mkubwa.
Hata hivyo, katika kutathmini hali hiyo, lazima
pia tuangalie upande wa pili wa shilingi. Tukiangalia historia ya vyama
hivyo tangu vilipoanzishwa kabla na baada ya uhuru, tutagundua kwamba
vyama hivyo vilikuwa na nguvu na ufanisi mkubwa kiasi kwamba baadhi ya
vyama hivyo vilikuwa tishio kubwa kwa Serikali kutokana na kuwa na
uongozi imara, rasilimali nyingi na ushawishi mkubwa.
Licha ya kuwa huru na kuwajibika kwa wanachama,
vyama hivyo vilithaminiwa na kupendwa sana kwa jinsi vilivyokuwa
vikiwawakilisha katika masoko ya dunia vikipigana kufa na kupona kupata
bei nzuri ya mazao ya wakulima kama kahawa, pamba, tumbaku na kadhalika.
Baadhi ya vyama vilikua na kuweza kugharamia mambo mengine kama elimu
kwa watoto wa wanachama, afya, miundombinu na kadhalika.
Ndipo Serikali ilipoingilia kati na kuvuruga vyama
hivyo kwa kupanga bei ya mazao, kudhibiti mapato, ushawishi na nguvu za
vyama hivyo. Ilitungwa Sheria ya Bunge ya kuvibana kisera na kimfumo na
Serikali kujiingiza moja kwa moja katika uteuzi wa viongozi wa kuratibu
shughuli zake kwa kutumia taratibu na sera zilizoasisiwa na chama
tawala. Huo ndio ulikuwa mwisho wa vyama vya ushirika nchini. Vyama
tunavyovishuhudia sasa sio vyama halisi, bali ni ‘photokopi’ ya vyama
halisi vilivyouawa na Serikali.